Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameitaka Wizara ya Fedha kufanya marekebisho ya sheria za ununuzi wa umma ili kuongeza kiwango cha thamani ya miradi inayoweza kutekelezwa na kampuni za Kitanzania, akipendekeza kiwango cha Sh bilioni 50 kipandishwe hadi zaidi ya Sh bilioni 100 au Sh bilioni 150.
Dkt. Mwigulu amesema kiwango cha Sh bilioni 50 kwa baadhi ya miradi kimekuwa kidogo kutokana na kukua kwa uchumi na kuongezeka kwa uwezo wa kampuni za ndani.
“Hii ya bilioni 50 imeshakuwa ya kawaida wekeni bilioni 100… au kama mnarekebisha sasa ikachukua muda, wekeni bilioni 150 Mambo yanaenda mbele. Tuwawezeshe Watanzania kushika uchumi wao,” amesema.
Amesema kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ni muhimu katika kuongeza ajira, kukuza sekta binafsi, kuongeza mapato na kupunguza umaskini nchini.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo, Septemba 3, 2026, wakati akifungua Kongamano la Tano la Kitaifa la Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati na Uwekezaji, lililofanyika Dodoma.
Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira ya kisera, kisheria na kiutendaji yatakayowawezesha Watanzania kushiriki moja kwa moja katika shughuli za uchumi.
“Tuwawezeshe Watanzania kushika uchumi wao hii ndiyo njia ya kuongeza ajira, kuongeza vyanzo vya mapato na kujenga sekta binafsi yenye nguvu,” amesema.
Amesema lengo la kuwawezesha Watanzania si kuwazuia wawekezaji wa nje, bali kuongeza uwezo wa kampuni na wananchi wa ndani ili nao wanufaike na fursa zinazotokana na rasilimali na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC), Gwakisa Bapala, amesema takribani wadau 600 wameshiriki kongamano hilo la siku mbili lililoanza Septemba 2, 2026.
Amesema washiriki wamejadili changamoto na fursa zilizopo katika miradi ya kimkakati na uwekezaji, pamoja na kupewa mbinu za kushiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na manunuzi ya umma.
Bapala amesema pamoja na Serikali kuweka mwongozo unaotaka angalau asilimia 30 ya wanufaika wa zabuni za manunuzi ya umma kuwa makundi maalum, ikiwemo vijana, bado ushiriki wa makundi hayo umebaki kuwa mdogo, ukiwa karibu asilimia moja pekee.
Amesema kongamano hilo limeweka maazimio yanayolenga kuwapa wadau mbinu za kunufaika na zabuni za manunuzi ya umma, fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali pamoja na maeneo mengine yanayotolewa na Serikali.
Kongamano hilo limefanyika chini ya kaulimbiu: “Ushiriki wa Watanzania ni Nguzo ya Uchumi Shindani na Jumuishi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



