Trump Atishia Kuijibu Iran Kwa Nguvu Baada Ya Mashambulizi Mapya

Rais wa Marekani, Donald Trump, ametishia kuchukua hatua kali dhidi ya Iran baada ya nchi hizo mbili kubadilishana mashambulizi ya kijeshi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha takribani mwezi mmoja.

Mvutano huo umeongezeka baada ya Marekani kushambulia vituo vya kurushia makombora vya Iran katika Kisiwa cha Larak, kilichopo kwenye eneo la kimkakati la Mlango wa Hormuz. Marekani ilisema mashambulizi hayo yalilenga vikosi vya Iran vilivyokuwa vikijiandaa kuweka mabomu ya baharini katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji.

Iran ilijibu kwa kurusha makombora kuelekea vituo viwili vya kijeshi vinavyotumiwa na Marekani nchini Jordan. Jordan ilisema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilifanikiwa kuyadungua makombora manane, huku hakuna majeruhi walioripotiwa katika vituo hivyo.

Baada ya mashambulizi hayo, Trump alitoa onyo kali dhidi ya Iran, akisema Marekani itajibu kwa nguvu.

Trump pia amesema mashambulizi hayo hayamaanishi kwamba Marekani imerejea kwenye vita kamili na Iran, akidai kuwa uwezo wa kijeshi wa Tehran umeathirika kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, kauli hizo zimeongeza hofu kwamba mapigano yanaweza kuongezeka tena baada ya kipindi ambacho Marekani ilikuwa ikitumia zaidi shinikizo la kiuchumi na vikwazo dhidi ya Tehran.

Kisiwa cha Larak kiko katika eneo la Mlango wa Hormuz, njia muhimu sana kwa biashara ya mafuta duniani.

Marekani imesema ilichukua hatua dhidi ya vituo vya Iran baada ya kubaini maandalizi ya kurushwa kwa mabomu ya baharini ambayo yangeweza kuhatarisha meli zinazopita katika njia hiyo.

Mvutano kuhusu Mlango wa Hormuz umeendelea kuwa sehemu muhimu ya mzozo huo, huku Iran ikisisitiza kuwa njia hiyo haiwezi kufunguliwa kikamilifu bila masharti yake kutekelezwa.

Licha ya kujibu mashambulizi ya Marekani, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Tehran haitafuti vita na kwamba kuendelea kwa mapigano hakutakuwa na manufaa kwa Iran, eneo la Mashariki ya Kati wala dunia kwa ujumla.

Pezeshkian pia amesema Iran iko tayari kurejea kwenye mchakato wa mazungumzo iwapo Marekani itatekeleza ahadi zilizowekwa katika makubaliano ya muda yaliyofikiwa mwezi Juni.

Katika hatua nyingine, Trump alichapisha kwenye mitandao ya kijamii video iliyodai kuonyesha mashambulizi dhidi ya Kisiwa cha Kharg, kituo muhimu cha mafuta cha Iran.

Hata hivyo, taarifa zilizothibitishwa zinaonyesha kuwa video hiyo ilikuwa imetengenezwa kwa kutumia teknolojia ya akili bandia (AI), na hakuna ushahidi kwamba shambulio hilo lilifanyika wakati huo.

Kwa sasa, macho yanaelekezwa kwa hatua itakayochukuliwa na Marekani baada ya Trump kuahidi kulipiza kisasi, huku Iran ikiendelea kusisitiza kuwa iko tayari kujibu iwapo itashambuliwa tena.