Mbeto: Jussa Usithubutu Kuwagombanisha Watanzania Kwa Utashi wa Kisiasa

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC ya CCM Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, amemtaka Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Ladu, kuacha kutumia misamiati ya Utanganyika na Uzanzibari kwa kile alichodai kuwa ni juhudi za kuwagawa na kuwagombanisha Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi zake Kisiwandui, Mbeto amesema Utanzania ni msingi wa umoja, mshikamano na udugu kati ya Watanganyika na Wazanzibari, ambao umeendelea kudumu kwa zaidi ya miaka 62 tangu Muungano wa mwaka 1964.

Mbeto amesema ameshangazwa na kile alichokiita mwenendo wa kisiasa wa Jussa wa kuibua tofauti kati ya wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar, akidai kuwa hatua hiyo ni aina ya “fitna za siasa za uke wenza.”

Mbeto amesema kwa wiki kadhaa Jussa amekuwa akijionesha kuwa na mapenzi makubwa kwa Zanzibar huku akiwakebehi wananchi wa Tanzania Bara, bila kuzingatia kuwa miongoni mwao wapo pia wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo.

Amedai kuwa mwenendo huo unalenga kujenga taswira kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anapendwa zaidi na Wazanzibari kuliko wananchi wa Tanzania Bara.
“Mwambieni Jussa aachane na aina ya siasa za uke wenza. Rais Dkt. Samia tangu aingie madarakani amekuwa kipenzi cha Watanzania wote. Aina ya uongozi wake haina tofauti na viongozi wenzake waliomtangulia,” alisema Mbeto.

Mbeto amesema Rais Samia si kiongozi wa Wazanzibari pekee, bali ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo hakuna haja ya kutumia tofauti za kisiasa na kimaeneo kujaribu kuwagombanisha wananchi.

Akizungumzia historia ya uongozi nchini, Mbeto amesema viongozi waliowahi kuongoza Tanzania hawakujifunga katika maeneo yao ya kuzaliwa, bali waliongoza nchi nzima.
“Julius Nyerere hakuwa Rais wa Butiama, Ali Hassan Mwinyi hakuiongoza Mangapwani wala Benjamin Mkapa hakuwa Rais wa Lupaso. Kadhalika, Jakaya Kikwete hakuitwa Rais wa Msoga, John Magufuli hakuitawala Chato na Dkt. Samia si Rais wa Kizimkazi,” alisisitiza.

Amesema mifano hiyo inaonesha umuhimu wa kutenganisha maeneo ambayo viongozi wamezaliwa na nafasi zao za kitaifa, akisisitiza kuwa viongozi wa Tanzania wamekuwa wakiongoza nchi nzima.

Mbeto amemtaka Jussa kutambua hatua ambayo Watanzania wamefikia katika kujenga umoja na mshikamano, akisema hakuna mtu wala kundi lenye uwezo wa kuwagawa na kuwarudisha katika hali ya kabla ya Muungano wa mwaka 1964.

Ameeleza kuwa fikra za kuamini Tanzania inaweza kugawanyika kwa misingi ya maeneo au tofauti za kisiasa ni “ndoto za mchana na njozi za jinamizi.”
“Jussa acha fikra mgando kwa kudhani utafanikiwa kuwagawa Watanzania kwa utashi wako wa kisiasa. Waulize baba na kaka zako waliojaribu kufanya mtihani huo walifikia wapi,” alisema.

Mbeto amesema vyama vya siasa vinaweza kuwa na mitazamo na misimamo tofauti, lakini tofauti hizo hazipaswi kutumiwa kama sababu ya kuwagawa wananchi kwa misingi ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema CCM, ACT-Wazalendo na vyama vingine vya siasa vina haki ya kuwa na tofauti zao za kisiasa, lakini hakuna sababu ya kutumia tofauti hizo kuwagonganisha viongozi au kuchochea migawanyiko miongoni mwa wananchi.
“Si Jussa, ACT-Wazalendo wala wenzake ambao wamewahi kuwa na upendo kwa CCM. Hivyo, majaribu yoyote ya kutaka kuwagonganisha viongozi au kuwafitini, ngoma hiyo itapasukia kwake,” alimaliza.