Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkuu wa wilaya Kigoma Dk.Rashid Chuachua ameongoza viongozi wa serikali za Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (RDC) na Burundi kuaga miili ya watu sita waliofariki katika ajali ya kuteketea kwa moto kwa meli ya Mv.Pasific kwenye bandari ya Kigoma usiku wa Agosti 28 mwaka huu
Miili hiyo imeagwa katika hospitali ya mkoa Kigoma Maweni na kusafirishwa kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambapo Mkuu huyo wa wilaya Kigoma akimwakilisha Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro alisema kuwa serikali ya mkoa Kigoma kwa niaba ya serikali ya Tanzania inatoa pole kwa ndugu,jamaa, marafiki na serikali ya DRC kwa kuondokewa na watu hao ambao walikuwa wakifanya kazi ya kusadia kusafirisha abiria na mali kutoka Tanzania kwenda DRC.
Dk.Chuachua alisema kuwa serikali ya Tanzania kupitia vyombo vya ulinzi na usalama na kikosi cha zimamoto walichukua hatua madhubuti kuhakikisha kwanza wanapambana na moto lakini pia kuhakikisha wanaokoa maisha na mwisho kutafuta miili ya watu waliokuwepo kwenye meli hiyo na kwamba mapenzi ya Mwenyezi Mungu yametimizwa hadi leo miili hii inaposafirishwa kwenda DRC kwa mazishi.
Kwa upande wake Katibu wa CCM mkoa Kigoma, Christopher Pallangyo akitoa salamu za Katibu Mkuu wa CCM,Dk,Asha Rose Migiro alisema kuwa chama kimeguswa na msiba huo na kinatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki na serikali ya DRC kwani nchi hizi mbili ni ndugu na marafiki tukishirikiana kwa mambo mengi kwa manufaa ya nchi hizo mbili na watu wake.
Naye Balozi Mdogo wa ubalozi wa Burundi mkoani Kigoma, Kekenwa Jeremeah alisema kuwa serikali ya nchi hiyo imaungama na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Tanzania kwani marehemu walikuwa wakifanya kazi ambayo imekuwa ikiziunganisha nchi hizo kupitia ziwa Tanganyika.
Akizungumza katika ibada hiyo ya kuaga miili Balozi mdogo wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika ubalozi mdogo wa DRC Kigoma, Loius Kinyamba alisema kuwa serikali ya nchi hiyo imepokea kwa masikitiko makubwa vifo vya mabaharia hao na inatoa pole kwa ndugu wa marehemu hao.
Pamoja na hilo Balozi huyo amesema kuwa watafuatilia kwa kina sababu za tukio hilo na kuchukua hatua lakini pia akitoa wito kwa manahodha na wamiliki wa meli kuhakikisha wanawasilisha majina ya abiria wote wanaosafiri kweny meli zao, aina ya mizigo wanayosafirisha na uzito wake wakieleza maeneo ambayo mizigo na abiria hao wanakwenda akieleza kuwepo kwa udhaifua wa kupatikana kwa taarifa muhimu za meli hiyo zinazpopata ajali.
Mwisho.




