HASARA YA MGOMO WA WAFANYAKAZI WA SEKTA YA USAFIRI WA ANGA NCHINI KENYA

 

Baada ya zaidi ya saa 18 za mazungumzo, wadau katika sekta ya usafiri wa anga nchini Kenya wamekubaliana kusitisha mgomo uliodumu kwa siku mbili.

Katika taarifa iliyochapishwa mapema Jumanne, Waziri wa Uchukuzi wa Umma nchini Kenya, Davis Chirchir, amesema: “Kufuatia makubaliano yaliyofikiwa, KAWU inatangaza kusitisha mgomo huo mara moja na kuwaelekeza wafanyakazi walioathirika kurejea katika majukumu yao ya kawaida.”

Kwa sasa, pande zote zimeahidi kujitolea kurejesha haraka shughuli za kawaida za usafiri wa anga, kudumisha amani ya viwanda na kutatua malalamiko yoyote yaliyosalia au yatakayojitokeza baadaye kupitia mazungumzo, upatanishi na mifumo iliyoanzishwa kisheria.

Hata hivyo, baadhi ya watu tuliozungumza nao wameeleza hofu ya kukumbwa na ucheleweshaji wa safari kutokana na safari nyingi kuahirishwa awali. Wengi wana hofu kuwa itachukua muda kabla ya hali ya kawaida kurejea.

Taarifa hii imekuja kama afueni kwa maelfu ya wasafiri waliokwama katika viwanja vya ndege si tu nchini Kenya bali pia katika maeneo mengine duniani. Maelfu ya wasafiri walikwama katika miji kama Doha, London na Johannesburg wakisubiri safari ambazo zilitarajiwa kutua Nairobi au kuunganishwa kupitia Nairobi, baada ya kuahirishwa kwa zaidi ya saa sita.

Kwa mujibu wa Chama cha Wahudumu wa Usafiri wa Anga nchini Kenya (KAAO), Shirika la Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA) na Shirikisho la Utalii nchini Kenya (KTF), hasara iliyopatikana katika siku mbili za mgomo huenda ikafikia dola bilioni moja za Marekani, sawa na ilivyoshuhudiwa mwezi Februari mwaka huu wakati Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege nchini Kenya (KAWU) kilipoitisha mgomo mwingine.

Kulingana na mwandishi huru na mtaalamu wa masuala ya uchumi, Julian Amboko, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) una umuhimu mkubwa kwa wasafiri wengi, hasa kutoka Afrika Magharibi ambao hutegemea Kenya Airways kwa usafiri wao. Kwa sababu hiyo, safari nyingi kutoka eneo hilo hupitia Nairobi, huku wengi wakitumia uwanja huo kuunganisha safari kuelekea Ulaya, Mashariki ya Kati, Asia na mataifa ya Kusini mwa Afrika.

Wengi wameulizia iwapo viwanja vingine vya ndege katika ukanda wa Afrika Mashariki vinaweza kuziba pengo linaloachwa wazi wakati wa matatizo kama yale yaliyoshuhudiwa nchini Kenya katika siku mbili zilizopita.

Kulingana na Amboko, ikiwa Kenya haitafanya juhudi za kupanua JKIA au kujenga uwanja mpya wa ndege, upanuzi wa viwanja vya ndege na ujenzi wa viwanja vipya katika mataifa jirani unaweza kuiondoa JKIA katika nafasi yake ya sasa kama kitovu kikuu cha usafiri wa anga katika ukanda huo kwa kuzingatia idadi ya wasafiri wanaopita katika uwanja huo kila siku.

Baada ya mazungumzo ya siku nzima, Waziri wa Uchukuzi wa Umma nchini Kenya, Davis Chirchir, alitangaza kwamba pande hizo zilikubaliana kuwa ada za wakala zinazoshikiliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA) zitarejeshwa kwa KAWU mara moja.

Kuhusu masuala ya Mkataba wa Majadiliano ya Pamoja (CBA) wa KCAA, Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) imejitolea kuwashirikisha wahusika ndani ya mfumo husika wa kisheria na kiudhibiti, kwa kuzingatia uwezo wa mashirika ya serikali yanayohusika kulipa.

Suala la mkataba wa utambuzi kati ya KAWU na Jambojet linasubiri maelekezo ya mahakama. Pande hizo zimesema zinaheshimu mchakato unaoendelea wa kimahakama na zitaendelea kuongozwa na matakwa yote ya kisheria na kiutaratibu yanayohusiana na suala hilo.

Huku mgomo ukisitishwa kwa sasa, pande husika zinatarajiwa kuendelea kufanya vikao vya kutatua malalamiko yaliyosalia ya wafanyakazi hao katika wiki chache zijazo.

Kwa sasa, kampuni kama Kenya Airways na Jambojet zimetangaza kurejelewa kwa safari za ndege, huku wasafiri wengi wakielekea viwanjani kuthibitisha iwapo wataweza kusafiri kwa muda uliopangwa.