Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kutumia utafiti, teknolojia na ubunifu kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, huku kikijivunia kupata hataza 16 za kimataifa.
Miongoni mwa bunifu zinazotekelezwa na chuo hicho ni matumizi ya panya buku katika kubaini kifua kikuu (TB), mabomu yaliyotegwa ardhini pamoja na nyara za Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Tihelwa Chibunda, amesema mafanikio hayo yanaonyesha namna tafiti zinazofanywa na chuo hicho zinavyoweza kubadilisha maisha ya wananchi na kuongeza tija katika sekta mbalimbali.
Amesema kwa sasa SUA inatekeleza miradi 172 ya utafiti katika maeneo tofauti, huku ikizalisha wastani wa machapisho 500 ya kitaalamu kwa mwaka katika majarida yanayotambulika kitaifa na kimataifa.
Kwa mujibu wa Prof. Chibunda, kupitia Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viumbe Hai Waharibifu, panya buku wamefundishwa kubaini TB kwa kutumia makohozi, huku teknolojia hiyo ikitumika pia kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kubaini usafirishaji wa nyara za Serikali.
Amesema SUA pia imefanya utafiti wa kutumia bundi kudhibiti panya waharibifu mashambani, hatua inayolenga kupunguza matumizi ya sumu za kemikali na kuhifadhi mazingira.
“Tunafanya tafiti mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto za wananchi, ikiwamo migogoro kati ya binadamu, mifugo na wanyamapori,” amesema.
Katika sekta ya elimu, Prof. Chibunda amesema idadi ya wanafunzi wa SUA imefikia 17,438 kutoka 15,479 mwaka 2022/2023, huku chuo kikiwa na programu 58 za shahada za uzamili na 32 za shahada za awali, pamoja na programu nyingine za ngazi mbalimbali.
Amesema ongezeko la wanafunzi limekwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu, ambapo kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), SUA inajenga majengo tisa ya kimkakati katika Kampasi za Morogoro na Mizengo Pinda mkoani Katavi.
Prof. Chibunda alisema ujenzi katika Kampasi ya Mizengo Pinda umefikia asilimia 93, huku Serikali ikiwa imetenga Sh bilioni 1.7 kwa ajili ya fidia kwa wananchi 197 waliopisha eneo la upanuzi wa kampasi hiyo.
Aidha amesema SUA imekamilisha Jengo Mtambuka la Mafunzo la Dkt. Samia Suluhu Hassan lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,205 kwa wakati mmoja, likiwa na maabara nane na madarasa nane, kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 11.7.
Amesema chuo hicho sasa kinalenga kukamilisha miradi ya HEET, kuimarisha utafiti na biashara ya bunifu, kuboresha maabara kwa viwango vya kimataifa pamoja na kuimarisha SUA Media, ikiwamo kurejesha SUA TV na kuongeza masafa ya 101.1 SUA FM ili elimu ya kilimo iwafikie wananchi wengi zaidi.
Mwisho

.jpeg)