Video: Makamu wa Rais Awataka Watumishi Kuachana na Kazi kwa Mazoea

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, amewataka watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuongeza bidii, ubunifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.

Ndejembi ametoa kauli hiyo leo alipofanya ziara yake ya kwanza katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, iliyopo Mtumba jijini Dodoma, ambapo alipokelewa na watumishi pamoja na Menejimenti ya Ofisi hiyo.

Amesema watumishi wa Serikali wanapaswa kubadili mtazamo na namna ya kutekeleza majukumu yao, huku kila mmoja akitakiwa kuwa mbunifu na kuweka mipango yenye kulenga kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Makamu wa Rais amewataka watumishi kutambua dhamana kubwa waliyonayo katika kuwahudumia Watanzania na kuhakikisha nafasi zao zinatumika kutoa huduma zenye thamani na kuleta tija kwa wananchi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika kulinda na kudumisha Muungano wa Tanzania kwa kuweka mipango endelevu itakayosaidia kutatua changamoto zinazoukabili Muungano, sambamba na kuwaelimisha wananchi kuhusu fursa zinazopatikana kupitia Muungano huo.

Katika eneo la mazingira, Mhe. Ndejembi amewataka viongozi na watumishi wa Ofisi hiyo kuweka mikakati endelevu ya kuimarisha ajenda ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira.

Amesema kampeni za upandaji miti na usafi wa majiji na miji zinapaswa kupewa msukumo zaidi, huku kukiwa na maandalizi ya nyenzo na mifumo itakayosaidia kuhakikisha juhudi hizo zinaendelea kwa muda mrefu.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mpango maalum wa kusaidia wananchi kuachana na shughuli za kila siku zinazochangia uharibifu wa mazingira na kuwawezesha kutumia njia mbadala zinazolinda mazingira.

Makamu wa Rais amesema utekelezaji wa mipango hiyo unahitaji ushirikiano, ubunifu na uwajibikaji kutoka kwa viongozi na watumishi wote ili kuhakikisha Serikali inafikia malengo yake na kutoa huduma bora kwa wananchi.