Na,Jusline Marco;Arusha
Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetoa mchango wa dola za Marekani 2,500 kwa ajili ya kusaidia safari waendesha baiskeli kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Patrick Mbundi amesema EAC iko tayari kuimarisha ushirikiano na waandaaji wa safari hiyo katika siku zijazo, ikiwemo kushirikiana katika uhamasishaji na upatikanaji wa rasilimali pale itakapowezekana huku akisisitiza kuwa ushiriki wa jamii katika masuala ya Muungano hauwezi kutegemea Sekretarieti ya EAC pekee, bali unahitaji watu na taasisi mbalimbali kuwa sehemu ya utekelezaji.
Akizungumza katika uzinduzi wa safari ya baiskeli ya Great African Cycling Safari, Msemaji wa Jumuiya hiyo Balozi Mbundi amesema Muungano wa Afrika Mashariki unapaswa kuwa wa wananchi na kuendeshwa kwa kiasi kikubwa na sekta binafsi, huku Serikali zikibaki na jukumu la kuweka mazingira wezeshi kupitia sera na mifumo ya kitaasisi.
Amesema kuwa Great African Cycling Safari 2026 ni mfano wa namna wananchi wanaweza kuwa sehemu ya moja kwa moja ya kujenga na kuimarisha Muungano wa Afrika Mashariki kupitia michezo, ushirikiano wa kijamii na shughuli zinazovuka mipaka ya nchi.
Ameongeza kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imesisitiza umuhimu wa wananchi, vijana, sekta binafsi na mashirika ya kiraia kushiriki kikamilifu katika kuimarisha na kumiliki mchakato wa ujumuishaji wa kikanda.
Aidha amesema hatua na mwitikio wa kuendeleza Muungano huo unapaswa kuanzia kwa wananchi wa Afrika Mashariki, huku akiwapongeza waandaaji wa Great African Cycling Team kwa kuonyesha kwa vitendo umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika mchakato wa ujumuishaji wa kikanda.
Kwa mujibu wa Balozi Mbundi amesema Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa EAC umetambua kuimarisha mwelekeo wa kijamii wa Muungano wa kikanda kuwa miongoni mwa malengo yake ya kimkakati ambapo chini ya mkakati huo, mshikamano wa kijamii kupitia utamaduni na michezo ni eneo la kipaumbele, ili kuendeleza programu za michezo za kikanda kupitia ushirikiano.
Pamoja na hayo amemshukuru mwendesha baiskeli kutoka Zimbabwe kwa kujiunga na safari hiyo na kuunga mkono mpango huo, huku akisema ushirikiano wa aina hiyo unaonesha namna michezo inavyoweza kuunganisha watu kutoka mataifa mbalimbali na kusema Sekretarieti ya EAC itaendelea kutafuta maeneo ya ushirikiano na waandaaji wa safari hiyo ili kuimarisha mpango huo na kuongeza mchango wake katika kuendeleza Muungano wa kikanda.
Balozi Mbundi amewataka washirika wa EAC, jamii, sekta binafsi na wadau wengine kuendelea kuwaunga mkono waendesha baiskeli katika safari yao, ambapo amesema wana jukumu muhimu la kufikisha ujumbe wa ujumuishaji wa kikanda kwa wananchi.
Sambamba na hayo amewataka waendesha baiskeli hao, kuendelea kubeba ujumbe wa umoja na mshikamano katika maeneo yote watakayopita huku akisisitiza kuwa tofauti za kimtazamo miongoni mwa watu au nchi si lazima ziwe kikwazo cha maendeleo, kwa kuwa watu wenye hatima moja wanaweza kujadiliana, kutofautiana na hatimaye kufikia suluhisho linalokubalika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwanzilishi wa GACS- Cycling Afrika John Bosco Balongo amesema kupitia mashirikiano hayo, GACS inatoa fursa ya kipekee ya kuunganisha sera, programu na taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na wananchi wa kawaida kwa kutumia Baiskeli ambayo inakuwa daraja kati ya EAC na watu wake.
John Bosco amesema Safari ya GACS-EAC Tour 2026 tayari imedhihirisha ushirikiano huo wa Afrika Mashariki ambapo safari hiyo imetoa fursa kwa wananchi, vijana, jumuiya, taasisi na vyombo vya usalama kushiriki katika mazungumzo na shughuli za kiutendaji zinazochangia ajenda ya mtangamano wa Afrika Mashariki.
Amesema hadi kufikia sasa, GACS-EAC Tour 2026 imedhihirisha kwamba wakati wananchi wanapewa fursa, wako tayari kushiriki katika mchakato wa mtangamano wa Afrika Mashariki ambapo Safari hiyo imelenga kupanda mawazo na kujenga mahusiano, sambamba na kutengeneza majukwaa kwa ajili ya vijana.
Sambamba na hayo GACS imeomba uungwaji mkono na ushirikiano kutoka kwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Utambuzi na Ushirikiano, Mfumo wa Uratibu kati ya GACS na EAC, Vilabu vya Ushirikiano wa EAC, pamoja na Mawasiliano ya Pamoja na Uhamasishaji wa Umma, Ushirikiano wa Mwaka Mzima ambapo amesema safari ya kila mwaka ya GACS itakuwa ni mpango wa kudumu ndani ya ajenda pana zaidi inayohusu ushirikishwaji wa wananchi, ushiriki wa vijana, hatua za kuhifadhi mazingira, na uelimishaji wa umma kuhusu ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Ameongeza kuwa kwa sasa wanachohitaji ni ushirikiano imara zaidi wa kitaasisi ili kusaidia kuigeuza safari hiyo kuwa vuguvugu endelevu la kikanda kwa kila kilomita wanayopita kwa baiskeli ni fursa ya mazungumzo, kwa kila shule wanayotembelea ni fursa na kwa kila mpaka wanaovuka ni ukumbusho kwamba hatima yao imeunganishwa hivyo kila kijana anayeshiriki ni balozi mtarajiwa wa ushirikiano wa Afrika Mashariki.



.jpeg)


.jpeg)