Shalulile Na Mudathir Waipeleka Yanga Kileleni, Yawafunga Fountain Gate 2-0

Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha umeshuhudia mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Fountain Gate FC na Yanga SC, ambapo Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kuendeleza rekodi yake ya ushindi wa asilimia 100 katika mechi tano za mwanzo za msimu.

Yanga ilianza mchezo kwa kasi, ikitafuta bao la mapema, huku Fountain Gate ikiwa makini katika dakika za mwanzo. Baada ya dakika kadhaa za kushambuliana, Peter Shalulile aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 26 baada ya kumalizia pasi ya kisigino kutoka kwa Stephane Aziz Ki, aliyecheza mechi yake ya kwanza ya ligi tangu kurejea Jangwani.

Bao hilo liliipa Yanga nguvu zaidi, huku mabingwa hao watetezi wakianza kutawala mchezo na kulazimisha Fountain Gate kutumia muda mwingi kujilinda.

Licha ya wenyeji kujaribu kusawazisha, safu ya ulinzi ya Yanga iliendelea kuwa imara na kuzuia mashambulizi yao, hivyo kipindi cha kwanza kikamalizika Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili, Yanga iliendelea kulisakama lango la Fountain Gate, huku benchi la ufundi likifanya mabadiliko kwa lengo la kuongeza nguvu katika eneo la kiungo na ushambuliaji.

Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 76, ambapo Mudathir Yahya alifunga bao la pili baada ya kufuatilia mpira uliorejea kutoka kwa kipa wa Fountain Gate, kufuatia shambulizi lililoanzishwa na Seleman Mwalimu.

Fountain Gate ilijaribu kutafuta bao la kufutia machozi katika dakika zilizobaki, lakini Yanga iliendelea kudhibiti mchezo hadi filimbi ya mwisho, na hivyo kuondoka Arusha na ushindi wa mabao 2-0.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 15 baada ya kushinda mechi zote tano, huku ikiwa imefunga mabao 15 na kuruhusu mawili pekee.

Kwa upande mwingine, Fountain Gate imebaki na pointi tatu baada ya mechi tano, ikiendelea kutafuta matokeo yatakayoiinua katika msimamo wa ligi.

FT: Fountain Gate 0-2 Yanga SC
⚽ 26′ Peter Shalulile
⚽ 76′ Mudathir Yahya