ZAIDI YA WATU 600 WAMEAGA DUNIA KUTOKANA NA MAFURIKO YALIYOTOKEA NEPAL – TIBET

 

Operesheni ya kuwatafuta manusura wa mafuriko nchini Nepal, imeingia siku ya nne baada ya mafuriko hayo kusababisha maafa katika mpaka wa Nepal na Tibet siku ya Jumatano.

Idadi ya waliofariki nchini Nepal imeongezeka na kufikia watu 626, kwa mujibu wa mamlaka za taifa hilo.

Watu 2,426 wanaripotiwa kutojulikana walipo.

Katika eneo la Tibet, idadi rasmi ya waliofariki imefikia saba, huku watu 554 wakiripotiwa kutojulikana walipo kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China.

Kupata taarifa kutoka Tibet imekuwa vigumu, lakini China sasa imetoa baadhi ya picha za tukio hilo.

Nchini Nepal, angalau raia 517 wa kigeni wameripotiwa kutoweka, wakiwemo mahujaji na watalii waliokuwa wakifanya safari za milimani.

Waziri wa Fedha wa Nepal amekadiria kuwa nchi hiyo itahitaji kati ya dola bilioni 4 au 5, kwa ajili ya kujenga upya taifa hilo baada ya mafuriko hayo makubwa.

“Haya ni makadirio tu. Tathmini ya hasara na uharibifu bado inaendelea,” Swarnim Wagle aliiambia shirika la habari la Reuters.