WATU WANNE WAFA MELI IKITEKETEA ZIWA TANGANYIKA

 

Na Fadhili Abdallah, Kigoma

Watu wanne wamekufa na wengine watatu hawajulikani walipo baada ya Meli ya Mv  Pacific waliyokuwa wakisafiria kuungua moto katika bandari ya Kigoma mkoani Kigoma.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma alisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia August 29 mwaka huu katika bandari ya Kigoma Mjini Kigoma.

Kamanda Makungu alisema kuwa mtu mmoja alipatikana usiku wa tukio na watu wengine watatu walipatikana  mchana August 29 wakati wazamiaji walipokuwa wakitafuta miili ya abiria waliokuwa ndani ya meli hiyo.

Meli hiyo iliyokuwa ikitoka Kigoma kuelekea Kalimie Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo pamoja na mizigo mingine ilikuwa imebeba lita 16,000 ya mafuta ya dizeli yaliyokuwa yamewekwa kwenye matanki ambapo meli hiyo ilikuwa maalum kwa kubeba mizigo.

Meli hiyo ya abiria ilikuwa imesajiliwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu alisema ilipata ajali ikianza safari kuelekea DRC na  kuwa uchunguzi wa chanzo cha ajali unaendelea na taarifa zaidi itatolewa.