RAIA WAWILI WA NIGERIA WAPELEKWA MAREKANI KUJIBU MASHTAKA YA UHALIFU WA MTANDAONI

 

Wanaume wawili kutoka Nigeria wamesafirishwa hadi nchini Marekani, kujibu mashtaka ya ulaghai wa kingono mtandaoni, katika sakata inayohusisha kifo cha kijana mmoja wa Marekani, kulingana na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).

Mkurugenzi wa FBI, Kash Patel, amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X ,kwamba wanaume hao raia wa Nigeria, walikamatwa baada ya uchunguzi kufanywa.

Shirika la Nigeria la Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kifedha (EFCC) liliwataja wanaume hao wawili kuwa Mudashiru Afeez Olawale na Adebola Festus Adekunle.

EFCC ilisema wawili hao walikabidhiwa kwa mamlaka za Marekani kufuatia uchunguzi wa FBI kuhusu madai ya kuwalaghai watoto.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye X, shirika hilo lilisema washukiwa hao wanadaiwa kuwalenga wavulana wenye umri wa kati ya miaka 13 na 17, wakitumia picha zao za uchi kuwalazimisha kutoa pesa kupitia kadi za zawadi, kuwatumia kwa benki na sarafu za kidijitali.

Kwa mujibu wa EFCC, kesi moja ilihusisha mvulana mwenye umri wa miaka 13 ambaye aliwasiliana na wawili hao kwenye mtandao wa Instagram na kubadilishana picha za uchi.

Shirika hilo lilisema baadaye mvulana huyo alitishiwa kuwa picha hizo zitasambazwa kwa watu wake wa karibu iwapo hangewatumia pesa.

“Vitisho hivyo viliendelea hata baada ya kijana huyo kusema kwamba alikuwa na nia ya kujiua,” EFCC ilisema.

Mitandao hiyo ya kuwalaghai watoto kwa kuwatishia kuvujisha picha zao za uchi zilichochea kifo cha mtoto mmoja, na uchunguzi ukapelekea kukamatwa kwa raia hao wawili wa Nigeria.