NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA, MWANZA
JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekitambua Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kuwa miongoni mwa wadau muhimu katika utekelezaji wa majukumu yake, hususani katika maeneo ya elimu, malezi na ustawi wa walimu na wanafunzi.
Hayo yamebainishwa wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Wazazi yaliyofanyika kitaifa Mkoani Mwanza, ambapo Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Magesa Protas Magesa, pamoja na viongozi wa CWT Mkoa wa Mwanza, wapoalikwa na kushiriki katika maadhimisho hayo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Magesa amesema CWT inafurahia kushirikiana na Jumuiya ya Wazazi, na kueleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu kutokana na majukumu yao yanayogusa kwa karibu masuala ya elimu na malezi ya watoto.
Amesema CWT kwa upande wake inasimamia na kutetea maslahi ya watumishi, hususani walimu, wakati Jumuiya ya Wazazi ikiwa inamiliki shule mbalimbali ambazo zina walimu wanaowakilishwa na CWT.
“Kwa upande wa Chama cha Walimu tunashughulika na maslahi ya watumishi, hususani walimu, lakini Jumuiya ya Wazazi ina shule mbalimbali ambazo zina walimu wetu. Sisi kama Chama cha Walimu tunakuwa walezi wa walimu na wanafunzi, kwa hiyo tunahusika kwa namna moja au nyingine katika masuala ya malezi,” amesema Magesa.
Amesema CWT itaendelea kutoa ushauri na maoni kuhusu namna bora ya kuboresha mazingira ya utumishi, huku ikihakikisha maslahi na ustawi wa walimu vinazingatiwa.
Amesisitiza kuwa ushirikiano huo unalenga pia kuhakikisha walimu wanatekeleza majukumu yao katika mazingira mazuri na kupata motisha ya kuendelea kutoa huduma bora ya elimu kwa wanafunzi.
Aidha, amesema CWT itaendelea kujenga ukaribu na Chama Cha Mapinduzi, akieleza kuwa Serikali iliyopo madarakani inaongozwa na sera na Ilani ya CCM, hivyo ni muhimu kwa chama hicho kufikishiwa maoni na mahitaji ya walimu kupitia njia zinazostahili.
“Tunahakikisha tunakaa karibu na Chama Cha Mapinduzi ili kuwapa maoni ambayo walimu wetu wanataka yafanyike, kuhakikisha huduma na utumishi wa walimu wetu unaenda vizuri na wao wanafurahia utumishi wao kwa miaka yote,” amesema.
Amesema CWT itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu na malezi, ili kuhakikisha masuala yanayowahusu walimu na wanafunzi yanapewa kipaumbele katika jitihada za kuboresha elimu nchini.
Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Kitaifa yaliyofanyika Mkoani Mwanza yamewakutanisha viongozi, wanachama na wadau mbalimbali, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika masuala ya elimu, malezi na maendeleo ya Taifa.


.jpeg)
