Na Matukio DaimaMedia
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umepunguza muda wa wastani wa kulipa madai ya vituo vya kutolea huduma za afya kutoka siku 120 hadi 50, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha uhusiano kati ya mfuko huo na watoa huduma.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, amesema mafanikio hayo ni sehemu ya maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mfuko huo, yakilenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali, kudhibiti matumizi na kuboresha mifumo ya utoaji huduma.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, Dkt. Isaka amesema mapato ya mfuko yameongezeka kwa asilimia 10.3, huku matumizi yakipungua kwa asilimia 10.
Amesema mabadiliko hayo yamesaidia kupunguza uwiano wa gharama za matibabu dhidi ya mapato kutoka asilimia 87 hadi 71, kiwango kinachokaribia asilimia 70 kinachotajwa kimataifa kuwa muhimu katika kuimarisha uimara wa mifuko ya bima ya afya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza NHIF kwa kutambua mchango wa wanahabari katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kujiunga na huduma za bima ya afya.
Balile amesema nafasi 100 za bima zilizotolewa kwa wanahabari ni fursa muhimu, huku akiahidi kuwa TEF itashirikiana na NHIF kubaini waandishi na wahariri wenye uhitaji ili waweze kunufaika na huduma hiyo kwa haraka.
Naye Mratibu wa Elimu kuhusu Bima ya Afya kwa Wote kutoka Wizara ya Afya, Said Makora, amesema Serikali inaendelea kuongeza watumishi wa afya ili kukidhi mahitaji yanayotarajiwa kuongezeka kutokana na utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Amesema katika ajira 5,000 zilizotolewa katika sekta ya afya, watumishi 808 wamepelekwa katika ngazi ya huduma za afya ya msingi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Hata hivyo, amesema Serikali inaendelea kukabiliana na upungufu wa wataalamu wa afya, hususan katika huduma za mama na mtoto pamoja na matibabu ya saratani.




