Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media DODOMA
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kutumia fursa za rasilimali za madini zilizopo nchini kupanua uwekezaji wake, kuongeza uzalishaji na kuimarisha mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa.
Mavunde amesema shirika hilo linapaswa kutumia ipasavyo fursa zilizopo katika miradi mbalimbali ya madini, ikiwemo dhahabu eneo la Kigosi, madini ya kimkakati mkoani Morogoro na nikeli mkoani Mtwara, ili kuongeza wigo wa shughuli zake na kuimarisha mapato.
Wito huo umetolewa wakati STAMICO ikiendelea kupanua shughuli zake katika sekta ya madini na nishati ya kupikia, ikiwemo kuzindua kiwanda chake kipya cha kuzalisha mkaa mbadala wa Rafiki Briquette jijini Dodoma.
Kiwanda hicho ni cha nne kwa shirika hilo tangu kuanza kwa uzalishaji wa bidhaa hiyo inayotokana na makaa ya mawe, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho, Mavunde alisema mkaa wa Rafiki Briquette una uwezo wa kuwaka kwa zaidi ya saa tatu na nusu, huku kilo moja ikiuzwa kwa Sh1,000.
Alilitaka shirika hilo kuhakikisha bidhaa hiyo inasambazwa kwa wingi na kupatikana kwa urahisi katika maeneo mbalimbali nchini, badala ya kubaki katika maeneo yanayozalishwa pekee.
Alisisitiza umuhimu wa STAMICO kuimarisha mfumo wa masoko kwa kushirikiana na wafanyabiashara na mawakala, akieleza kuwa uzalishaji unapaswa kwenda sambamba na mikakati madhubuti ya kuwafikia watumiaji.
“Mtumizi ya nishati hiyo ni sehemu ya mchango wa sekta ya madini katika kufanikisha lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,” Amesema Waziri Mavunde.
Akizungumzia mabadiliko ya shirika hilo, Mavunde alisema miaka mitano iliyopita STAMICO lilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyotathminiwa kwa uwezekano wa kufutwa kutokana na kutokuwa na tija, lakini sasa limefikia mapato ya zaidi ya Sh bilioni 89 kutoka Sh milioni moja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasilwa, amesema kiwanda cha Dodoma kimejengwa kwa kuzingatia nafasi ya mji huo kama makao makuu ya nchi pamoja na mahitaji ya nishati safi katika mkoa huo na maeneo jirani.
” Shirika limejenga mtandao wa mawakala 92 nchini, wakiwemo 35 kutoka taasisi ya Wanawake na Samia Tanzania, kwa lengo la kurahisisha usambazaji wa bidhaa hiyo, “.
Na Kuongeza”Katika uzinduzi huo wamekabidhiwa pia magari madogo aina ya toyo 30 na makontena kwa ajili ya kuwezesha usafirishaji na uuzaji wa Rafiki Briquette katika maeneo mbalimbali, ” Amesema
Dkt. Mwasilwa amesema wazo la kuzalisha bidhaa hiyo lilitokana na utafiti ulioanza mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2022, huku bidhaa hiyo ikipata cheti cha ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Amesema STAMICO inaendelea na maandalizi ya kujenga kiwanda kingine mkoani Geita ili kuongeza uzalishaji na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Mbali na uwekezaji katika nishati ya kupikia, amesema shirika hilo limeagiza mitambo 10 ya uchorongaji madini kwa lengo la kuimarisha shughuli za utafiti na kuongeza ajira kwa vijana.
Ameeleza kuwa kila mtambo mmoja unatarajiwa kutoa ajira kwa vijana takribani 50, hivyo mitambo yote ikianza kufanya kazi itatoa fursa za ajira kwa vijana takribani 500.
Naye mwakilishi wa taasisi ya Wanawake na Samia Tanzania Fatuma Madidi alisema wanawake wamepata fursa ya kuwa mawakala wa bidhaa hiyo katika maeneo mbalimbali nchini na wamejipanga kuhakikisha inawafikia watumiaji wengi zaidi.
Amesema STAMICO imewawezesha kupata makontena na vifaa vya usafirishaji, hatua itakayowasaidia kushiriki katika biashara ya nishati safi ya kupikia na kuchangia utekelezaji wa lengo la taifa la matumizi ya nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.





