Ikulu Yakanusha Taarifa za Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Mambo ya Nje Kujiuzulu

WASHINGTON, MAREKANI: Ikulu ya Marekani imekanusha taarifa zinazodai kuwa Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, na Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio, wanatarajiwa kuondoka katika nyadhifa zao kufuatia mabadiliko yanayoweza kufanyika ndani ya utawala wa Rais Donald Trump baada ya chama cha Republican kupata pigo kubwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula.

Taarifa hizo zimeibuka wakati kukiwa na shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wa Republican wanaotaka Hegseth aondolewe madarakani, wakimhusisha na namna alivyoshughulikia vita vya Iran, ambavyo vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia kushindwa kwa chama hicho katika uchaguzi.

Hata hivyo, Hegseth ameonesha kutokuwa tayari kuondoka, akichapisha ujumbe wa video uliolenga kutetea utendaji wake na kupinga juhudi za kumwondoa madarakani.

Katika ujumbe huo, Hegseth alisema mashambulizi dhidi yake yanatokana na mafanikio ya kazi anayoifanya, akisisitiza kuwa hataacha kutekeleza majukumu yake.

Kwa upande wake, Rubio amekanusha taarifa zinazodai kuwa anafikiria kujiuzulu ili kujiandaa kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2028.

Akizungumza na gazeti la The New York Times, Rubio alisema mpango wake umekuwa kuendelea kufanya kazi katika utawala wa Trump hadi mwisho wa muhula wake.

Alieleza kufurahishwa na majukumu yake ya sasa, huku akizitaja taarifa za kuondoka kwake kuwa za kuchekesha.

Ikulu ya Marekani pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje nazo zimekanusha taarifa hizo, zikizitaja kuwa habari zisizo za kweli.

Hata hivyo, mustakabali wa kisiasa wa Hegseth unaonekana kukabiliwa na changamoto zaidi kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la kutaka aondolewe katika nafasi hiyo.

Rais Trump na Makamu wake, JD Vance, wamehusisha vita vya Iran na matokeo mabaya ya Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula, ambapo chama cha Democratic kimefanikiwa kupata udhibiti wa Baraza la Wawakilishi na Seneti ya Marekani.

Katika mahojiano ya simu na kituo cha televisheni cha ABC News, Trump alikiri kupokea simu kutoka kwa watu waliokuwa na maoni kuhusu Hegseth, lakini akasema bado ana nia ya kumuacha aendelee na wadhifa wake.

Baadaye, akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu, Trump alimsifu Hegseth kwa kile alichokiita utendaji mzuri, akitaja baadhi ya mafanikio ambayo anayaunganisha na uongozi wake, yakiwemo kukamatwa kwa kiongozi wa Venezuela, Nicolás Maduro, mwezi Januari na mwenendo wa vita vya Iran.

Wakati huo huo, gazeti la The Washington Post limeripoti kuwa Trump anaweza kuwa anafikiria kuwaondoa pia Jenerali Dan Caine, Mwenyekiti wa Wakuu wa Majeshi ya Marekani, au Admirali Brad Cooper, Mkuu wa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), ambao walikuwa na nafasi muhimu katika kutoa ushauri kuhusu vita vya Iran.

Shinikizo dhidi ya Hegseth limeongezeka zaidi baada ya Mbunge wa Republican, Thomas Massie, kutangaza kuwa ataendelea na mpango wa kuwasilisha hoja ya kumuondoa waziri huyo madarakani kupitia mchakato wa impeachment.

Massie ameiambia tovuti ya Politico kuwa anatarajia kuanzisha hatua hiyo mapema wiki ijayo.

Kupitia mtandao wa X, mbunge huyo pia amemtaka Trump kumteua mtu mwingine kuchukua nafasi ya Hegseth kabla ya Bunge jipya linalodhibitiwa na Democrats kuanza kazi Januari.

Amesema hatua hiyo ingempa Rais nafasi ya kupata uthibitisho wa Seneti kuhusu uteuzi wa mrithi wa Hegseth kabla ya mabadiliko ya uwiano wa kisiasa ndani ya Bunge.

Kwa upande mwingine, Hegseth pia amekuwa akitajwa kuhusishwa na uwezekano wa kuwania nafasi ya wazi ya uwakilishi wa jimbo la Tennessee katika Seneti ya Marekani.

Katika kujibu juhudi za kutaka aondolewe madarakani, Hegseth amezitaja tuhuma za impeachment kuwa ni njama za kisiasa zinazoendeshwa na mbunge aliyeshindwa kisiasa pamoja na washirika wake wa Democratic.

Ametetea utendaji wa Wizara ya Ulinzi chini ya uongozi wake, akitaja kuongezeka kwa juhudi za kuajiri wanajeshi, kujenga upya sekta ya uzalishaji wa vifaa vya kijeshi na kuondoa programu za utofauti ndani ya jeshi.

Hegseth amewashutumu wapinzani wake kwa kutumia majukwaa ya kisiasa kushambulia viongozi badala ya kujikita katika sera.

Kwa sasa, Trump ameonesha kumuunga mkono Hegseth, huku Ikulu ikisisitiza kuwa hakuna mpango uliotangazwa wa kuwaondoa mawaziri hao wawili katika nafasi zao, licha ya kuendelea kwa mijadala kuhusu mabadiliko ya uongozi ndani ya utawala wake kufuatia matokeo ya uchaguzi.