– *Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi yataka kampuni hiyo kukubaliana na jamii kuhusu miradi mbadala ya kiuchumi na gharama zake*
DODOMA: Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi imeipa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Polygold siku 30 kukamilisha maboresho ya Mpango wa Ufungaji Mgodi wake.
Kamati hiyo pia , imeitaka Polygold kukutana na Kamati ya Wilaya ya Ufungaji Migodi (DMCC) ya Musoma ndani ya wiki mbili ili kukubaliana kuhusu miradi ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi wanaozunguka mgodi huo baada ya shughuli za uchimbaji kukoma.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha mpango wa ufungaji mgodi wa kampuni hiyo unaainisha kwa kina miradi mbadala ya shughuli za kiuchumi (Alternative Livelihood Projects), itakayoiwezesha jamii kuendelea kujipatia kipato na kujenga uchumi endelevu hata baada ya mgodi kusitisha uzalishaji.
Akizungumza Novemba 5, 2026, katika ukumbi wa Tume ya Madini jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu wa Migodi nchini, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema kampuni hiyo inapaswa kushirikiana na Kamati ya Wilaya kubaini aina ya mradi unaokidhi mahitaji ya jamii, gharama zake na namna utakavyotekelezwa.
Amesema maelekezo hayo yametolewa baada ya Kamati ya Kitaifa kupitia Mpango wa Ufungaji Mgodi uliowasilishwa na Polygold na kubaini mapungufu, hususan katika kipengele kinachohusu miradi ya maendeleo kwa jamii pamoja na gharama za utekelezaji wake.
Mhandisi Kamando amesema kampuni hiyo, kwa kushirikiana na Kamati ya Wilaya ya Ufungaji Migodi ya Musoma, inapaswa kukamilisha majadiliano ndani ya wiki mbili kuanzia Novemba 5, 2026, na kuwasilisha mapendekezo ya mradi utakaokuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Aidha, ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha gharama za utekelezaji wa mradi wa jamii zinajumuishwa katika gharama kuu za ufungaji mgodi, huku ikiendelea kufanya maboresho ya mpango mzima na kuuwasilisha Tume ya Madini ndani ya siku 30 kwa ajili ya hatua zaidi.
Kwa upande wake, uongozi wa Kampuni ya Polygold umeahidi kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo na kukamilisha maboresho ya mpango wa ufungaji mgodi ndani ya muda ulioelekezwa.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Kitaifa ya Ufungaji Migodi imesisitiza umuhimu wa kampuni zote za uchimbaji madini kuhakikisha mipango yao ya ufungaji migodi inaainisha miradi mbadala ya kiuchumi kwa jamii zinazozunguka migodi, ili wananchi wasipoteze vyanzo vyao vya mapato mara baada ya shughuli za uchimbaji kukoma.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Madini, Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi Bora ya Ardhi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma pamoja na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara.
…….
