Global Publishers
November 5, 2026
72 views
0 Comments

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, leo Novemba 5, 2026 amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeipa uzito ajenda ya upatikanaji wa Katiba Mpya, akieleza kuwa dhamira ya kufufua mchakato huo ipo na tayari mwongozo umetolewa.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu, aliyetaka kufahamu ni lini mchakato wa Katiba Mpya utaanza pamoja na utaratibu utakaotumika katika utekelezaji wake.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema suala la Katiba Mpya ni muhimu kwa Watanzania na limejumuishwa katika Ilani ya Uchaguzi, jambo linaloonesha kuwa Serikali inalipa kipaumbele.
Amesisitiza kuwa Serikali ina dhamira ya kuendeleza suala hilo, huku akibainisha kuwa tayari hatua za kutoa mwongozo zimechukuliwa ili kuweka msingi wa kufufua mchakato huo.
Kauli hiyo imekuja wakati suala la Katiba Mpya likiendelea kuwa miongoni mwa ajenda muhimu katika mijadala ya kisiasa na kijamii nchini Tanzania, huku wananchi wakisubiri ufafanuzi zaidi kuhusu muda na utaratibu wa kuanza kwa mchakato huo.
