NA MATUKIO DAIMA MEDIA
IRINGA.Serikali imesisitiza umuhimu wa kulinda usalama na uhuru wa waandishi wa habari nchini ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na bila vitisho, huku ikivitaka kutumia ipasavyo taaluma yao kwa kuzingatia miiko na maadili ya uandishi wa habari katika kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini, hususan za kiuchumi na uwekezaji.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kukomesha kutoadhibiwa kwa wahalifu dhidi ya waandishi wa habari ,kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), mkoani Iringa.
Akifungua kikao hicho kilichowakutanisha wawakilishi wa klabu za waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali, Heri James alisema serikali inatambua mchango wa vyombo vya habari katika kuhabarisha umma na kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa taifa.
“Waandishi wa habari wanapaswa kupata mazingira rafiki yatakayowawezesha kuripoti mafanikio na changamoto za jamii kwa uhuru, huku wakizingatia weledi, usahihi wa taarifa na uwiano wa kimaadili”alisema na kuongeza kuwa
“vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kulinda haki, amani na mshikamano wa taifa,kuwa taarifa sahihi na zenye uwiano zinaweza kusaidia kupunguza uvumi, kuondoa kutokuelewana na kujenga uelewa miongoni mwa makundi mbalimbali ya kijamii”
Awali, Katibu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, alisema hali ya usalama wa waandishi wa habari nchini inaendelea kufuatiliwa kwa karibu, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za kulinda uhuru wa habari na kuhakikisha wanahabari wanafanya kazi katika mazingira salama yanayoheshimu haki na misingi ya taaluma hiyo.
Sungura alisema MCT inaendelea kufuatilia matukio ya ukiukwaji wa haki na vitisho dhidi ya waandishi wa habari ili kutathmini hali halisi ya usalama wao na kubaini changamoto zinazohitaji hatua za pamoja kutoka kwa wadau wa sekta ya habari.
Kwa mujibu wa takwimu alizowasilisha, matukio 12 ya ukiukwaji wa haki dhidi ya waandishi wa habari yalikuwa yamethibitishwa katika kipindi cha mwaka 2026 , ikilinganishwa na matukio 51 yaliyoripotiwa mwaka 2025 na matukio 33 yaliyorekodiwa mwaka 2024.
Aidha, Sungura alieleza kuwa pamoja na umuhimu wa kulinda usalama wa waandishi wa habari wanapotekeleza majukumu yao, masuala ya mazingira ya ajira bado ni changamoto inayohitaji kushughulikiwa ili kuimarisha uhuru na weledi wa taaluma hiyo.
Alibainisha kuwa takwimu zilizotajwa zinaonyesha asilimia 62 ya waandishi wa habari barani Afrika hawana mikataba rasmi ya ajira, huku hali ya Tanzania ikitajwa kuwa na changamoto kubwa zaidi, ambapo takwimu za kipindi cha miaka mitatu iliyopita zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya waandishi wa habari hawana mikataba rasmi ya ajira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa UTPC Keneth Simbaya amewataka Wadau wa masuala ya ajira na haki za binadamu kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha usalama na ustawi wa waandishi wa habari, kwa kuweka mfumo rasmi utakaosaidia kubaini changamoto na vihatarishi vinavyowakabili pamoja na kuboresha usimamizi wa haki zao.
Simbaya alisema kuwa maamuzi yanayofikiwa Novemba 2, 2026 yameweka msingi muhimu wa kuimarisha usalama wa waandishi wa habari, huku akisisitiza umuhimu wa kutathmini maeneo ambayo tayari yanafanya vizuri na yale yanayohitaji kuongezewa nguvu ili kupata matokeo bora zaidi.
“Masuala ya usalama wa waandishi wa habari si jukumu la kundi moja pekee, bali ni suala linalohusu jamii nzima na linahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali, kwa kuwa changamoto zinazowakabili waandishi zinaweza kuwa na athari pana zinazogusa haki za binadamu, demokrasia na jamii kwa ujumla.
Aidha, amesema rasimu ya mfumo huo inalenga kuweka utaratibu usioegemea upande wa kisiasa utakaoleta uwiano na mwendelezo katika kushughulikia masuala ya waandishi wa habari, kubaini vihatarishi vinavyowakabili na kuziba mapengo yaliyopo katika usimamizi wa haki na usalama wao.
Kikao hicho kinatarajiwa kusaidia wadau wa habari kutathmini changamoto zinazowakabili waandishi wa habari na kuweka mikakati ya kuimarisha usalama wao, uhuru wa habari na mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Peter Kivuyo kutoka ofisi ya kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa kitengo cha dawati la sheria na upelelezi alisema kuwa waandishi wa habari wanaowajibu wa kutekeleza majukumu yao bila woga wala vitisho kwa sababu jeshi hilo lipo kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi na mali zao.
MWISHO.
