Matukio Daima Media, Morogoro
Juhudi za kuwafikia watoto wenye ulemavu wa kichwa kikubwa na mgongo wazi mkoani Morogoro zimepata msukumo kupitia huduma za madaktari bingwa zinazoendelea kutolewa katika Zahanati ya Polisi, zikilenga kubaini mahitaji ya matibabu na kuwaunganisha watoto na huduma stahiki.
Zoezi hilo lililoanza Oktoba 20 mwaka huu limehusisha madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi.
Katika watoto 58 wenye hali hiyo, watoto 10 wamepatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Dkt. Hamis Shabani,ni daktari bingwa wa upasuaji kutoka MOI, amesema uchunguzi wa watoto hao ni muhimu ili kubaini mahitaji yao ya kiafya na kuwawezesha kupata matibabu yanayofaa.
Akasema wamekuwa wakiangalia afya za watoto hao kila baada ya miezI mitatu, lakini kwa hao 51 wa Morogoro hawakuwa wamerudi MOI kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dkt. Christina Guveti, amesema kuboresha upatikanaji wa huduma kwa watoto wenye ulemavu ni muhimu ili kupunguza vikwazo vinavyokwamisha familia kupata matibabu kwa wakati.
Francis Duwe ambaye ni miongoni mwa watoto wenye changamoto hiyo amebainisha kuwa ukosefu wa vifaa saidizi na gharama kubwa za matibabu ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amesisitiza umuhimu wa jamii kuondoa ubaguzi na kuwapa watoto hao upendo, ushirikiano na msaada wanaohitaji.
Mwisho






