Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema uzinduzi wa majengo ya ofisi, wizara, taasisi za Serikali na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ni hatua muhimu katika kuimarisha utendaji wa Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali yenye miundombinu bora, mazingira rafiki ya kazi na huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma Oktoba 27, 2026, Prof. Kabudi amesema maendeleo ya miundombinu katika Mji wa Serikali Mtumba yanaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha shughuli za Serikali zinafanyika katika mazingira yanayoongeza ufanisi.
Amesema Mji wa Serikali Mtumba ni utekelezaji wa azma ya muda mrefu ya Serikali ya kuhamishia shughuli zake Dodoma na kujenga mazingira bora yatakayowezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
“Chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuweka mkazo katika kukamilisha na kuboresha miundombinu ya Mji wa Serikali Mtumba na Makao Makuu, ” Amesema Prof Kabudi.
Prof. Kabudi amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
“Uwepo wa wizara na taasisi katika eneo moja unatarajiwa kurahisisha uratibu wa shughuli za Serikali, mawasiliano baina ya taasisi, utoaji wa huduma pamoja na utekelezaji wa majukumu ya kitaifa,” Amesema Prof Kabudi
Amesema hatua hiyo pia itapunguza changamoto za kutawanyika kwa ofisi za Serikali katika maeneo mbalimbali na kuongeza ufanisi katika utendaji wa shughuli za Serikali.
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amesema ujenzi wa barabara za lami ndani ya Mji wa Serikali Mtumba ni hatua muhimu katika kuendeleza mji huo kwa kuimarisha usafirishaji, mawasiliano na upatikanaji wa huduma.
Amesema barabara hizo zitasaidia kurahisisha usafirishaji, mawasiliano na upatikanaji wa huduma, sambamba na kuunganisha maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mji wa Serikali.
Ameeleza Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutoa msukumo mkubwa katika kukamilisha miradi mbalimbali ya kimkakati nchini, ikiwemo Mji wa Serikali Mtumba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha maendeleo ya taifa.
AmesemaUtekelezaji wa miradi hiyo unaelezwa kuwa ishara ya dhamira ya Serikali ya kujenga Taifa lenye miundombinu ya kisasa na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Prof. Kabudi amesema Mji wa Serikali Mtumba unaendelea kuwa moja ya alama muhimu za utekelezaji wa dhana ya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali, huku ukiendelea kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.
Aidha, uwekezaji huo unatarajiwa kuleta fursa kubwa kwa sekta binafsi na wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazochochewa na ukuaji wa Mji wa Serikali na Makao Makuu.
Hata hivyo amehimiza watumishi wa umma wanaofanya kazi katika Mji wa Serikali Mtumba kutumia vizuri miundombinu iliyopo na kuhakikisha mazingira hayo yanachochea uwajibikaji, nidhamu ya kazi na uzalendo ili wananchi wapate huduma bora.
Katika kuadhimisha uzinduzi huo, wananchi wa Mkoa wa Dodoma wamealikwa kushiriki katika shughuli za uzinduzi wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami Oktoba 30, 2026.
“Siku hiyo pia itatambuliwa kwa kutangazwa kuwa siku maalumu ya upigaji wa fataki usiku wa tarehe 30 Oktoba, 2026, ambapo wananchi watapata burudani na kufurahia wakati wa kuelekea tukio la uzinduzi, ” Amesema
Prof. Kabudi amesema uzinduzi wa majengo hayo ni hatua muhimu katika safari ya kuifanya Mji wa Serikali Mtumba kuwa kitovu cha kisasa cha shughuli za Serikali nchini, huku akiishukuru jamii, watendaji, wakandarasi na wadau wote walioshiriki katika utekelezaji wa programu hiyo.








