DAR ES SALAAM: Baadhi ya mawakili ambao ni wanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) wamefungua shauri la kikatiba katika Mahakama Kuu kupinga mchakato wa kinidhamu dhidi ya Rais wa chama hicho, Boniface Mwabukusi, ambao unaweza kusababisha kuvuliwa uwakili.
Mawakili hao wamesema mchakato wa kumfikisha Mwabukusi mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili unazua maswali kuhusu uhuru wa TLS na utekelezaji wa maamuzi yanayotolewa na wanachama wa chama hicho.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mawakili hao wamesema hatua yao ya kisheria inalenga kulinda uhuru wa chama hicho na kuhakikisha kinaendelea kutekeleza wajibu wake katika kusimamia masuala ya sheria nchini.
Akizungumza kwa niaba ya mawakili hao, Wakili Jebra Kambole amesema tuhuma zinazomkabili Mwabukusi zinatokana na kauli alizotoa katika Mkutano Mkuu wa TLS wa mwaka 2026 kuhusu mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Kambole amesema kauli hizo ziliungwa mkono na wanachama wa TLS, ambao waliagiza uongozi wa chama hicho kutoa tamko rasmi kwa waandishi wa habari ndani ya saa 48 kuhusu mashtaka yanayomkabili Lissu.
Amesema Mwabukusi alikuwa akitekeleza wajibu wake kama Rais wa TLS kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa na wanachama katika mkutano huo.

Kwa upande wake, Wakili Paul Kisabo amesema mawakili hao wamechukua hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo kufungua shauri la kikatiba Mahakama Kuu, kupinga mchakato wa kinidhamu unaoendelea dhidi ya Mwabukusi.
Mawakili hao wanadai kuwa suala hilo haliishii kwa Mwabukusi kama mtu binafsi, bali linagusa pia uhuru na nafasi ya TLS kama taasisi ya kitaaluma inayopaswa kutoa ushauri kwa serikali na jamii kuhusu masuala ya kisheria.
Wamesisitiza kuwa hawatakubali kile walichokitaja kuwa ni kuingiliwa kwa uhuru wa chama hicho, wakieleza kuwa hatua yao ya kisheria inalenga kulinda uwezo wa TLS kutekeleza majukumu yake bila kuathiriwa na shinikizo linaloweza kuzuia utekelezaji wa maamuzi ya wanachama wake.
Shauri hilo linatarajiwa kuwa sehemu ya hatua za kisheria zinazolenga kupinga mchakato huo, huku hoja kuu ya mawakili hao ikiwa ni kulinda uhuru wa TLS na nafasi yake katika kusimamia utawala wa sheria nchini.
