Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WALIMU mkoani Kigoma wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuendana na mabadiliko ya utendaji kazi kwa kutumia mfumo wa teknolojia ya habari kwa kufanya kazi zao mbalimbali ikiwemo maandalio ya masomo na utoaji wa taarifa na takwimu za shughuli walizofanya.
Kaimu Afisa Elimu wa mkoa Kigoma, Fausta Akaro alisema hayo katika maadhimisho ya siku ya walimu kwa mkoa Kigoma yaliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la serikali ya Ubelgiji (ENABEL) kupitia mradi wake wwa wezesha binti.
Akaro alisema kuwa kwa sasa shughuli nyingi za utendaji wa serikali zinafanyika kwa kutumia mfumo wa tenkolojia ya habari na mawasiliano ambao walimu kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuendana nao ikiwemo kuingiza mahudhuria ya wanafunzi madarasani ambao Mkuu wa shule na idara ya elimu ya halmashauri ikiingia kwenye mfumo inaona taarifa hizo bila kumpigia simu mwalimu.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Shule ya elimu ya chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk.Eugenia Kafanabo alisema kuwa wakati huu ambao dunia inasherehekea siku ya walimu ni vizuri jamii ikaungana na kuwapongeza walimu kwa kazi kubwa, nzuri na ngumu wanayofanya kwa wanafunzi ambao wanabeba jukumu la malezi ya watoto kama wazazi.
Dk.Kafanabo alisema kuwa ni lazima jamii ihimizwe kuheshimu taaluma ya ualimu ili kuwakumbusha wanafunzi, wazazi, maafisa wa serikali, na jamii kwamba ualimu ni taaluma tukufu na hivyo walimu wanapaswa kupongezwa na kutiwa moyo ili wafanye makubwa zaidi ya hayo wanayofanya kwa manufaa ya wanafunzi na taifa kwa jumla.




