ACT WAZALENDO YATAKA ELIMU BURE, YALAANI GHARAMA ZA USAJILI NA UPUNGUFU WA MIKOPO

 

Na Matukio DaimaMedia 

ACT Wazalendo kimetaka Serikali kuhakikisha elimu inakuwa bure kuanzia elimu ya awali hadi shahada ya kwanza, kikieleza kuwa gharama kubwa za usajili vyuoni na upungufu wa mikopo ya elimu ya juu vinawanyima wanafunzi wengi fursa ya kuendelea na masomo.

Katika tamko lililotolewa Oktoba 11, 2026, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa chama hicho, Riziki Shahari Mngwali, amesema sera ya ACT Wazalendo ni Serikali kuwajibika kugharamia elimu ya umma badala ya kuwaachia wazazi na wanafunzi mzigo wa gharama za masomo na madeni ya mikopo.

ACT Wazalendo imesema kati ya waombaji 157,309 wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2026/2027, wanafunzi 84,180 pekee wamepangiwa mikopo katika awamu ya kwanza, huku 73,129 wakikosa.

Aidha, chama hicho kimeeleza kuwa gharama mbalimbali za kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) zimeongezeka kutoka Shilingi 97,400 hadi Shilingi 255,400, sawa na ongezeko la Shilingi 158,000. Ada ya kitambulisho imepanda kutoka Shilingi 5,000 hadi 15,000, huku gharama za mitihani zikiongezeka kutoka Shilingi 12,000 hadi 30,000.

Kutokana na hali hiyo, ACT Wazalendo imetaka Serikali kufuta mfumo wa mikopo kwa ajili ya ada, utafiti na mahitaji ya kimasomo, na badala yake kugharamia mahitaji hayo kwa wanafunzi wote waliodahiliwa katika vyuo vikuu na vyuo vya kati. HESLB ibaki kutoa mikopo ya kujikimu kwa chakula na malazi.

Chama hicho kimesisitiza kuwa upatikanaji wa elimu haupaswi kutegemea uwezo wa kifedha wa familia, kikitaka Serikali kuongeza bajeti kwa vyuo vikuu vya umma na kupitia upya gharama zinazotozwa wanafunzi ili kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa anapata fursa ya elimu bila vikwazo vya kifedha.