Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo amewezesha viongozi wa kata zote 18 za jimbo hilo kushiriki mafunzo ya itikadi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yanayofanyika kuanzia Oktoba 9 hadi 19, 2026.
Ngajilo amechukua jukumu hilo ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kufanikisha mafunzo hayo yanayolenga kuimarisha chama kuanzia ngazi za chini.
Mafunzo hayo yanawalenga makada na viongozi wa CCM katika ngazi za kata na matawi, yakilenga kuongeza uelewa wa itikadi ya chama, kuongeza wanachama, kujenga uwezo wa kisiasa na kimaadili, pamoja na kuwawezesha viongozi wa chama kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Akizungumzia mchango huo, Diwani wa Kata ya Igumbiro, Jack Chatanda, amempongeza mbunge huyo kwa moyo wake wa kujitolea na kuunga mkono shughuli za chama.
Chatanda amesema Ngajilo amekuwa akisaidia shughuli mbalimbali za CCM, ikiwemo vikao vya ngazi za wilaya na kata, kila anapowasilishwa maombi ya msaada.
“Nadhani amekuwa mwepesi kusaidia chama kwa kuwa amelelewa na chama tangu akiwa Chipukizi, hivyo ana mapenzi ya dhati,” alisema Chatanda.
Kwa upande wao, viongozi wa CCM katika kata mbalimbali za Iringa Mjini wamempongeza Ngajilo kwa mchango wake, wakieleza kuwa hatua hiyo inaonesha kujali na kuthamini shughuli za chama.
Wamesema mchango huo utasaidia kurahisisha ushiriki wa kata zote 18 katika mafunzo hayo na kuimarisha maandalizi ya viongozi na makada watakaoshiriki.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa wa itikadi, maadili na misingi ya CCM miongoni mwa viongozi na wanachama wake katika Jimbo la Iringa Mjini.
Mwisho

