
Zaidi ya watu 30 wanadaiwa kufariki dunia katika ajali mbili tofauti zilizotokea usiku wa kuamkia leo, Oktoba 9, 2026, mkoani Morogoro, huku watu wengine 37 wakinusurika. Miongoni mwa wanaodaiwa kupoteza maisha ni askari wa Jeshi la Polisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Andrew Kantimbo, amethibitisha kutokea kwa ajali hizo, akieleza kuwa ajali ya kwanza ilitokea eneo la Miti Bora, kati ya Dakawa na Dumila, wilayani Mvomero, majira ya saa 6:45 usiku wa Oktoba 8, 2026.

Ajali hiyo ilihusisha gari lililokuwa na askari wa Jeshi la Polisi na gari jingine, ambapo watu wanne wanadaiwa kufariki dunia.
Ajali ya pili imetokea eneo la Mkambarani, maarufu kama Kikombe cha Chai, wilayani Morogoro, majira ya saa 10:30 usiku wa Oktoba 8, 2026, baada ya basi la abiria la Greenline lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Iringa kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba mbao, likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam.
Kutokana na mgongano huo, basi hilo liliteketea kwa moto, huku watu kadhaa wakihofiwa kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Joseph Mwasabeja, amesema kikosi chake kilifanikiwa kukamilisha zoezi la kuopoa miili ya marehemu na kusaidia kuwafikisha majeruhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.
Mwasabeja amesema awali jeshi hilo lilituma gari moja la zimamoto katika eneo la tukio, lakini baada ya kubaini ukubwa wa ajali hiyo, magari mengine mawili yaliongezwa ili kuimarisha shughuli za uokoaji na kuzima moto.

“Awali tulitoa gari moja liende eneo la tukio, lakini tukaambiwa ajali hiyo siyo nyepesi kama tunavyodhani. Tukaongeza magari mengine mawili. Kufika, hali ilikuwa mbaya, tayari moto ulikuwa umeshika kila sehemu,” amesema Mwasabeja.
Ameeleza kuwa kipaumbele cha jeshi hilo kilikuwa kuokoa maisha ya watu, huku juhudi za kuzima moto na kuokoa mali zikiendelea kulingana na mazingira ya tukio.
Hata hivyo, taarifa zaidi kuhusu idadi kamili ya vifo, majeruhi na chanzo cha ajali hizo zinatarajiwa kutolewa na mamlaka husika.
