Farida Mangube Matukio app Morogoro
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Jaji mstaafu Joseph Sinde Warioba, amesisitiza kuwa ukuaji wa sekta ya kilimo nchini unapaswa kwenda sambamba na kuboreka kwa maisha ya wakulima.
Jaji Warioba ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati akizungumza na wanajumuiya wa SUA katika Mahafali ya 48 ya Chuo hicho, akisema pamoja na Tanzania kujitosheleza kwa chakula, wakulima bado wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi na wanaishi katika mazingira magumu.
Amesema hali hiyo inapaswa kuwafanya wasomi na watafiti kutafuta majibu yatakayosaidia kuboresha maisha ya wakulima kwa kutumia tafiti, maarifa na ubunifu unaozalishwa katika vyuo vya elimu ya juu. Amesisitiza kuwa mafanikio ya kilimo hayapaswi kupimwa kwa kuongezeka kwa uzalishaji pekee, bali pia kwa kuangalia namna mkulima anavyonufaika kiuchumi.
Mwenyekiti wa Baraza la SUA, Andrew W. Massawe amesema katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake Katika kilimo na mazingira, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeanzisha Taasisi ya Mabadiliko ya Tabianchi na Bioanuai, itakayolenga kuimarisha utafiti, ubunifu na teknolojia za kutafuta suluhisho zitakazolinda rasilimali za asili na kuongeza tija na ustahimilivu wa kilimo nchini.
Amesema pamoja na hatua hiyo, SUA imeendelea kutekeleza miradi 116 ya utafiti katika maeneo mbalimbali nchini, inayolenga kuzalisha maarifa, teknolojia na ubunifu wa kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Raphael Chibunda, amesema Chuo hicho kimeendelea kuimarisha utafiti, ubunifu na mafunzo yanayolenga kujibu changamoto za Taifa, hususani katika sekta ya kilimo.
Profesa Chibunda amesema miongoni mwa hatua zilizopigwa ni kupata idhini ya Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) kwa SUA kuendesha programu ya kikanda ya Shahada ya Umahiri ya Sayansi katika Uhandisi na Usimamizi wa Umwagiliaji.
Amesema programu hiyo, ambayo itadahili wanafunzi kutoka nchi za Afrika Mashariki, itaiimarisha SUA kuwa kitovu cha kikanda cha kuzalisha wataalamu wa umwagiliaji, ambao ni muhimu katika kuongeza uzalishaji na tija ya kilimo, hasa katika kukabiliana na changamoto za utegemezi wa mvua.
Aidha, Profesa Chibunda amesema Chuo kinaendelea kutekeleza Mradi wa Mabadiliko ya Kiuchumi katika Elimu ya Juu (HEET) kwa lengo la kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia na kufundishia, huku zaidi ya watumishi 226 wakiendelea na mafunzo ya umahiri na uzamivu ndani na nje ya nchi.
Amesema hatua hizo zinaenda sambamba na kuanzishwa kwa programu mpya tano za masomo na kuanza kwa shughuli za Kampuni ya Uzalishaji Mapato na Huduma za Chuo, hatua zinazolenga kuongeza uwezo wa SUA katika kutoa elimu yenye tija, kujitegemea kifedha na kuchangia maendeleo ya Taifa.





