RAIS SAMIA APELEKA TABASAMU KWA WASANII TOZO ZIKIPUNGUZWA

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetangaza marekebisho ya kanuni ambazo zimepunguza utitiri wa tozo na kupunguza kwa kiwango kikubwa kiwango cha ada walizokuwa wakitozwa wasanii na wanaofanya shughuli za sanaa kwa mwaka.

Hayo yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Edward Buganga wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu marekebisho hayo ya kanuni.

Alisema marekebisho ya tozo hizo kwa mwaka 2026 yalifanywa na Bunge zinazolenga kuimarisha usimamizi wa Sanaa, kuwawezesha wasanii na wadau wa Sanaa, na kupunguza utitiri wa tozo.

Alisema kanuni hizi ambazo tayari zimeanza kutumika na tunawakumbusha wadaua kuwa hazilengi kuzuia ubunifu na zinaweka utaratibu unaolinda wasanii, hadhira, watoto, urithi wa Sanaa na maslahi ya wadau, huku ikiwezesha sekta kukua na kushindana ndani na nje ya nchi.

 Alisema mabadiliko hayo ya kanuni yanahusu wasanii na vikundi vya Sanaa, maDJs, washereheshaji, maproduza, Mameneja,  Waandaaji wa Matukio, Studio na Kampuni za Sanaa, Vyombo vya habari vinavyotumia Wasanii na Kazi za Sanaa, Vyama na Mashirikisho, Wamiliki wa Kumbi, Wasambazaji wa kazi za Sanaa na wadau wengine wa Sanaa.

Alisema kwa mujibu wa kanuni hizo mpya, msanii huru anapotaka kujisajili kwa mara ya kwanza analazimika kulipa shilingi 10,000 na kuhuisha kibali chake kila mwaka atalipia shilingi 10,000 tofauti na zamani ambapo walikuwa wakilipa shilingi 40,000.

Alisema tozo za vikundi vya sanaa zilikuwa shilingi 60,000 kwa mwaka lakini kwa sasa zimepunguzwa hadi shilingi 30, 000 wanaposajili na watakapotaka kuhuisha vibali vyao kila mwaka watalazimika kutoa tena shilingi 30,000.

Buganga alisema mwandaaji wa tukio la sanaa atalazimika kuomba kibali kwa BASATA siku 30 kabla ya tukio lake na kwamba kibali hicho sasa kitatolewa bila malipo.

“Hapa tunasisitiza waandaaji wa matukio ya sanaa wawe na vibali ili wataalamu wetu wawasaidie kuwapa mwongozo wa Kwenda vizuri na kibali atapata bure, akikiuka tutamchukulia hatua,” alisema

Alisema kanuni zimegusia usajili na utoaji wa vibali, upunguzaji wa baadhi ya tozo, usimamizi wa sanaa katika Mikoa na Wilaya, usalama wa matukio na kumbi za Sanaa, ulinzi wa watoto katika sanaa, ulinzi wa sanaa za jadi na urithi, maadili, nidhamu na mazingira bora na nafuu kwa shughuli za Sanaa.

Buganga alisema usajili na vibali vitatolewa kupitia mfumo wa kidijitali wa AMIS na kwamba mwombaji akitimiza masharti, cheti au kibali hutolewa ndani ya siku saba na huwa halali kwa muda wa mwaka mmoja.

Kuhusu matukio ya sanaa, Buganga alisema matukio yoye ya sanaa yanahitaji kuwa na kibali cha BASATA Pamoja na mpango wa tukio ambavyo vinatakiwa kuwasilishwa angalau siku 30 kabla.

“Mwandaaji anatakiwa kuhakikisha wasanii na wahusika wote wana vibali halali, usalama wa washiriki na hadhira unazingatiwa, na maudhui yanazingatia sheria na Maadili ya mtanzania,” alisema.

Alisema kazi za sanaa hazipaswi kuchochea vurugu, ubaguzi, unyanyasaji au kukiuka sheria na badala yake sanaa inaweza kuelimisha, kukosoa, kuonya na kuelekeza jamii na kwamba ukosoaji wa kijamii si kosa iwapo unazingatia sheria na Maadili.

Akizungumzia ulinzi wa sanaa za jadi, alisema matumizi ya Sanaa za jadi kwa madhumuni ya kibiashara nje ya muktadha wa jamii husika yatahitaji kibali cha BASATA.

Alisema hatua hiyo inalenga kulinda urithi, utamaduni na haki za jamii zinazomiliki na kurithisha Sanaa hizo na kwamba mapato yatakayopatikana kupitia matumizi ya Sanaa Jadi yatarejeshwa kwa jamii husika kwenye eneo la Sanaa.

Kuhusu wasanii wa nje na maonesho nje ya nchi, Buganga alisema msanii au kikundi kinachokwenda nje ya nchi kwa maonesho kinahitaji kuwa na kibali cha BASATA na kuwasilisha taarifa ndani ya kabla ya safari.

“Wasanii wa kigeni wanaokuja Tanzania kwa shughuli za kibiashara watahitaji kuwa na  kibali cha BASATA. Shughuli za mafunzo, warsha, kubadilishana ujuzi au kidiplomasia zinaweza kupewa utaratibu maalumu wa kutotozwa ada, kwa mujibu wa Kanuni,” alisema .

Mwisho