Na Matukio DaimaMedia
Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA) limeanza mchakato wa kuridhia somo la msingi la Akili Mnemba (AI) litakalotumika katika vyuo vikuu vya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uelewa wa matumizi, fursa, changamoto na maadili ya teknolojia hiyo.
Hatua hiyo imefanyika kupitia warsha iliyowakutanisha wataalamu na makamishna wa elimu ya juu kutoka nchi wanachama wa EAC kwa ajili ya kupitia na kuthibitisha maudhui ya somo hilo kabla ya kuanza kutumika katika programu mbalimbali za elimu ya juu.
Akizungumza katika warsha hiyo, Kaimu KatibuMkuu wa Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA), Profesa Idris Rai, amesema somo hilo litawawezesha wanafunzi kutumia Akili Mnemba kwa ufanisi katika kufanya maamuzi, ufundishaji, ujifunzaji na tafiti, huku wakizingatia usalama, maadili na miongozo inayohitajika.
Amesema mpango huo pia unalenga kuwaandaa vijana wa Afrika Mashariki kuwa wabunifu na watengenezaji wa mifumo ya Akili Mnemba inayozingatia mahitaji, utamaduni na mazingira ya Afrika, badala ya kuwa watumiaji wa teknolojia zinazotengenezwa nje ya ukanda huo.
Profesa Rai amesema somo hilo linatarajiwa kutumika katika taaluma mbalimbali, zikiwemo Sheria, Tiba, Lugha na Uhandisi, ili kuwapa wanafunzi na walimu ujuzi wa kutumia teknolojia hiyo katika maeneo yao ya kitaaluma.
Kwa upande wake, Afisa Udhibiti Ubora Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Dkt. Mariam Issa Hamisi, amesema TCU inashirikiana na IUCEA kuandaa kozi za msingi za Akili Mnemba, huku ikihakikisha matumizi yake katika vyuo vikuu yanazingatia viwango vya ubora, maadili na kulinda hadhi ya taasisi.
Amesema teknolojia hiyo tayari imeanza kuwa muhimu katika elimu na inatumika katika taaluma mbalimbali, ikiwemo Kiswahili, Historia na Udaktari, katika ufundishaji, ujifunzaji na tafiti.
Naye Mshauri wa Sera za Akili Mnemba Afrika Mashariki kutoka GIZ, Evelyn Elliseus Rutazala, amesema shirika hilo linashirikiana na IUCEA kujenga uwezo wa vyuo vikuu na taasisi binafsi ili Afrika Mashariki iwe na wataalamu wanaoweza kutengeneza na kutumia teknolojia hiyo kwa kuzingatia mahitaji ya ukanda.
Mhadhiri na Kaimu Mkuu wa Idara ya Sayansi za Kompyuta wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Daniel John Ngondya, amesema UDOM inashiriki katika kuimarisha matumizi ya Akili Mnemba kupitia nafasi yake kama kituo cha AI (AI Node), ikishirikiana na vyuo vingine kuboresha ufundishaji na tafiti.
Mpango huo unawezeshwa na Serikali ya Ujerumani kwa kushirikiana na EAC, ukiwa na lengo la kuimarisha uwezo wa Afrika Mashariki kutumia Akili Mnemba katika elimu, uchumi, tafiti, ubunifu na maendeleo ya ukanda.
