MKUU mpya wa Wilaya ya Ileje, Kapenjama Ndile, amesisitiza matumizi sahihi na yenye tija ya fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri, akisema zinapaswa kuelekezwa katika miradi na huduma zilizokusudiwa kwa manufaa ya wananchi.
Ndile aliyasema hayo, Oktoba 5, 2026, wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ileje, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Community Center, Itumba.
Hafla hiyo ilifanyika baada ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi, kukabidhi rasmi ofisi kwa Ndile, kufuatia uhamisho wake kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ndile alimpongeza Mgomi kwa utendaji wake uliosaidia kusukuma mbele maendeleo ya Wilaya ya Ileje, akisema ataanzia pale alipoishia ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Alisema mshikamano na ushirikiano kati ya viongozi, watendaji na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha Ileje inaendelea kufanya vizuri katika nyanja mbalimbali na kuboresha ustawi wa wananchi.
Ndile pia alisema atafanya kazi kwa bidii na kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kutekeleza kwa ufanisi azma ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Alisisitiza kuwa fedha za Serikali na mapato ya ndani ya Halmashauri ni rasilimali za wananchi, hivyo zinapaswa kutumika kwa uangalifu na kuelekezwa katika vipaumbele vilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mgomi aliwashukuru viongozi, watendaji na wananchi wa Ileje kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chake cha uongozi, huku akiwaomba kuendelea kumpa ushirikiano Mkuu mpya wa Wilaya.
Mgomi alisema licha ya kuhamia Mbozi, bado yuko tayari kushirikiana na Ileje kwa kuwa wilaya hizo zote zipo ndani ya Mkoa wa Songwe, akisisitiza kuwa maendeleo hayana mipaka ya kiutawala na Tanzania ni nchi moja.
