Kibaha yaimarisha upimaji ardhi kupunguza migogoro
Kibaha. Manispaa ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, kuimarisha hatua ya upimaji na urasimishaji wa ardhi kupitia wataalamu wake ili kuharakisha upatikanaji wa hati za umiliki na kupunguza migogoro inayotokana na kutokuwa na nyaraka halali.
Hatua hiyo inakuja baada ya baadhi ya wazabuni waliokuwa wamepewa kazi za upimaji na urasimishaji kushindwa kukamilisha kazi hizo, hali iliyowaacha baadhi ya wananchi waliolipia huduma hizo bila hati za ardhi.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Manispaa ya Kibaha Agosti 19, 2026, Meya wa Manispaa hiyo, Dk Nicas Mawazo, amesema uamuzi huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za upimaji na urasimishaji kwa wakati.
Amesema awali manispaa ilikuwa ikiwatumia wazabuni kutekeleza kazi hizo, lakini baadhi yao hawakukamilisha kazi walizopewa, hali iliyochangia wananchi kukosa hati na kuongeza uwezekano wa kutokea kwa migogoro ya ardhi.
“Baada ya uhakiki kukamilika, shughuli ya urasimishaji itaanza ili kila mwananchi awe na hati na kunufaika na ardhi yake, huku Serikali nayo ikinufaika kupitia kodi ya ardhi,” amesema Dk Mawazo.
Amesema uhakiki wa wananchi waliotoa fedha kwa ajili ya urasimishaji lakini hawakupata huduma hiyo tayari umeanza na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Agosti mwaka huu.
Kwa mujibu wa Dk Mawazo, hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi waliokuwa wamesubiri kwa muda mrefu wanapata huduma walizolipia na kuwa na uhakika wa umiliki wa maeneo yao.
Amesema kuwa na hati za ardhi kutawasaidia wananchi kutumia maeneo yao kwa shughuli mbalimbali za maendeleo, huku Serikali ikiongeza mapato kupitia kodi ya ardhi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk Rogers Shemwelekwa, amewataka wananchi kushirikiana na wataalamu wa ardhi katika shughuli hiyo ili ikamilike kwa wakati.
Amesema ushirikiano huo utasaidia kutoa taarifa sahihi kuhusu maeneo, kutambua wamiliki halali na kurahisisha mchakato wa upimaji na urasimishaji.
Baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, huku wakitaka manispaa kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda sambamba na ahadi zilizotolewa.
Charles John amesema uamuzi huo umewapa matumaini wananchi waliokuwa wakingojea huduma hiyo kwa miaka kadhaa.
Amesema anafurahishwa na hatua ya manispaa kuanza kushughulikia changamoto hiyo, lakini ameitaka ifuatwe na vitendo ili wananchi waliolipia huduma wapate haki zao.
Naye Anitha John amesema upimaji na urasimishaji wa ardhi ni muhimu kwa sababu humpa mwananchi uhakika wa umiliki na kumwezesha kutumia ardhi yake kwa shughuli za maendeleo.

