Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Close

Search

  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Subscribe
Habari

UNDP: Vyuo geuzeni tafiti kuwa biashara kutengeneza ajira

By admin
August 19, 2026 3 Min Read
Comments Off on UNDP: Vyuo geuzeni tafiti kuwa biashara kutengeneza ajira

Arusha. Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limezitaka taasisi za elimu ya juu nchini kuacha kuishia kuzalisha tafiti kwa ajili ya machapisho ya kitaaluma, badala yake zigeuzwe kuwa bidhaa, huduma na biashara zitakazotatua changamoto za jamii, kuzalisha ajira na kuchochea uchumi.

Wito huo umetolewa leo, Agosti 19, 2026, na Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara, wakati akizungumza na wanafunzi wanaotarajia kuhitimu elimu ya juu katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) jijini Arusha, kuelekea mahafali ya 12 ya taasisi hiyo.

Komatsubara amesema Tanzania inapolenga kufikia uchumi wa kipato cha kati, haiwezi kuendelea kutegemea sekta za jadi pekee, bali inahitaji kuharakisha mabadiliko kuelekea uchumi unaotegemea maarifa, utafiti, teknolojia na ubunifu.



Amesema vyuo vikuu vina nafasi kubwa katika mabadiliko hayo kwa kuwa ni vyanzo muhimu vya maarifa na teknolojia zinazoweza kutumika kutatua changamoto za nchi na kuibua fursa za kiuchumi.

“Tafiti zinazofanywa maabara zinapaswa kubadilishwa kuwa suluhisho zilizo tayari kwa matumizi na soko, si kuishia katika machapisho ya kitaaluma pekee,” amesema Komatsubara.

Amesema endapo tafiti zinazozalishwa vyuoni zitafikishwa kwenye soko, zinaweza kuwa chanzo cha bidhaa na huduma mpya, kuongeza uzalishaji na kutoa ajira kwa vijana, badala ya maarifa hayo kubaki kwenye mazingira ya kitaaluma pekee.

Komatsubara pia amewataka wahitimu kubadili mtazamo kuhusu ajira kwa kuacha kujiona kama watafutaji wa ajira pekee, bali kuwa wabunifu na watengenezaji wa fursa.

Amesema teknolojia, ujasiriamali, kilimo cha kisasa, teknolojia za kijani na huduma za kifedha za kidijitali ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kuibua ajira ambazo hazipo kwa sasa.

“Ajira bora mnayoitafuta huenda bado haipo. Huenda ikazaliwa kupitia kizazi chenu, shauku yenu na ubunifu wenu, hivyo nendeni mkawekeze nguvu kutengeneza ajira, si kusaka zilizotengenezwa na wengine,” amesema.

Kwa mujibu wa Komatsubara, utafiti na teknolojia zinazozalishwa nchini zinapaswa kuwa na matokeo yanayoonekana katika viwanda, kilimo, huduma za kifedha, mazingira na uchumi wa kijani, badala ya kubaki kwenye kabati za vyuo.

Amesema hatua hiyo ni muhimu pia katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2050, inayolenga kujenga uchumi wenye tija, ushindani na unaotegemea maarifa na ubunifu.

Amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu, Serikali, sekta binafsi na wajasiriamali ili tafiti zinazozalishwa ziwafikie walengwa na hatimaye kuingia sokoni.

“UNDP itaendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha vipaji, ujuzi na ubunifu, pamoja na kusaidia kujenga mazingira ya kupata mitaji na kuharakisha biashara ya tafiti na bunifu,” amesema.

Amesema shirika hilo pia litaendelea kusaidia kuharakisha biashara ya tafiti na ubunifu, ikiwamo kupitia wiki ya ubunifu inayofanyika nchini kila mwaka.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula, amesema mkusanyiko huo umelenga kuwaunganisha wahitimu watarajiwa na waliowahi kuhitimu ambao wamefanikiwa kutumia tafiti na bunifu zao kutatua changamoto za jamii, kuanzisha biashara na kutengeneza ajira.

Amesema NM-AIST inalenga kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kubadilisha tafiti kuwa suluhisho zinazotumika katika jamii, viwanda na uchumi.

“Tanzania haiwezi kubaki kuwa mtumiaji wa teknolojia zinazozalishwa nje ya nchi. Tunapaswa kujenga uwezo wa ndani wa kuunda, kuboresha na kufanya biashara ya teknolojia zinazokidhi mahitaji yetu,” amesema.

Profesa Kipanyula amesema mustakabali wa Tanzania na Afrika hautategemea kiasi cha maarifa kinachozalishwa pekee, bali uwezo wa kuyageuza maarifa hayo kuwa suluhisho, ajira, biashara na ustawi wa jamii.

Amesema kwa kufanya hivyo, vyuo vya elimu ya juu vinaweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto ya ajira kwa vijana, huku vikichangia kuongeza uzalishaji na ushindani wa uchumi wa Taifa.

Amewataka wahitimu kutumia maarifa waliyopata kwa uadilifu, ubunifu na ujasiri katika kutatua changamoto zinazoikabili Tanzania, Afrika na dunia.

Amesema shahada wanazopokea hazipaswi kuwa mwisho wa safari yao, bali mwanzo wa kutumia maarifa yao kuleta mabadiliko katika jamii.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

Kibaha yaimarisha upimaji ardhi kupunguza migogoro

Next

Saratani ya mlango wa kizazi yaongoza kwa vifo nchini

Recent Posts

  • Pande mbili utekelezaji agizo la Chalamila kuhusu malori
  • Saratani ya mlango wa kizazi yaongoza kwa vifo Tanzania
  • Makandarasi, kampuni za ujenzi walalamikia faini TRA
  • Waziri wa zamani wa Ukraine ataka uchaguzi vitani
  • Tanzania yaikabidhi DRC vifaa tiba vya Sh220 milioni kukabili Ebola

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
  • Magazeti
  • Michezo
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme