Ujumbe muhimu kwa malezi ya mtoto

Written by

in

Dar es Salaam. Mtoto anayekulia katika mazingira yenye kila kitu, akipewa simu ya kisasa, kusoma shule nzuri na kushiriki burudani mbalimbali, bado anaweza kukosa maarifa muhimu ya maisha ikiwa hajawahi kukutana na mazingira yanayomsaidia kuelewa dunia inayomzunguka.

Wataalamu wa saikolojia wanaeleza kuwa kabla mtoto hajafikisha miaka 13, mzazi ana nafasi kubwa ya kumjengea uwezo wa kufikiri, kuuliza maswali, kufanya uamuzi, kuwa na huruma na kuelewa tofauti za maisha kupitia uzoefu wa moja kwa moja.

Badala ya kusubiri mtoto awe kijana ndipo aanze kujifunza kuhusu fedha, kazi, historia, utamaduni na maisha ya watu wengine, wazazi wanashauriwa kutumia miaka hiyo kumpeleka katika maeneo mbalimbali.

Maktaba inaweza kuwa lango la mtoto kuelekea dunia ambayo hawezi kuiona katika mazingira yake ya kawaida.

Kumpeleka maktaba humfundisha kuwa maarifa hayapatikani kupitia simu au mwalimu pekee, bali pia kupitia vitabu na kujisomea.

Makumbusho nayo humkutanisha na historia, sanaa, utamaduni na simulizi za jamii mbalimbali.

Akizungumza na Mwananchi, mwanasaikolojia Amina Msuya anasema uzoefu huo hujenga udadisi na uwezo wa mtoto kuuliza maswali badala ya kukubali kila jambo bila kutafakari.

Shamba, soko na supermarket

Mzazi anashauriwa kumpeleka mtoto shambani ili aone chakula kinapotoka kabla hakijafika mezani.

“Aone mbegu ikipandwa, mazao yakitunzwa na kuvunwa. Hii humsaidia kuthamini kazi na chakula badala ya kuona kila kitu kinapatikana kwa urahisi,” anasema Amina.

Katika soko, mtoto anaweza kujifunza biashara, mawasiliano na namna watu wanavyotafuta kipato, huku supermarket ikiwa darasa la fedha.

Mtaalamu wa uchumi, Jesca Magolanga, anasema mzazi anaweza kumpa mtoto kiasi maalumu cha fedha na kumruhusu achague bidhaa, hatua inayomsaidia kujifunza bajeti, kufanya uchaguzi na kujizuia kununua vitu vinavyopita uwezo wake.

Ziara ya benki inaweza kuwa mwanzo wa mazungumzo kuhusu kuweka akiba, matumizi na kupanga fedha.

Kadhalika, mtoto akipelekwa mahali mzazi au ndugu anapofanya kazi anaweza kuona uhusiano kati ya elimu, ujuzi, kazi na kipato.

“Mtoto anapopewa fursa ya kuona watu wakifanya kazi, huanza kuelewa mapema kuwa mafanikio yanahitaji juhudi, nidhamu na uwajibikaji,” anasema Jesca.

Hospitali, zimamoto na polisi

Hospitali inaweza kumfundisha mtoto umuhimu wa afya, huruma na kuwathamini watu wanaowahudumia wengine.

Kituo cha zimamoto kinampa nafasi ya kuona watu wanaokabiliana na hatari kwa ajili ya kuwaokoa wengine, huku kituo cha polisi kikimsaidia kuelewa usalama, sheria, wajibu wa raia na kujiepusha na vitendo vya uhalifu.

Hata hivyo, wataalamu wanashauri ziara hizo zifuatane na maelezo yanayoendana na umri wa mtoto ili zisijenge hofu, bali uelewa.

Mtoto anaweza kujifunza kuhusu imani, maadili, huduma na mshikamano kupitia ziara katika nyumba ya ibada.

Akizungumzia hilo, Sheikh Khamis Mataka anasema ni muhimu kwa wazazi kuwapeleka watoto kwenye nyumba za ibada ili wajifunze matendo mema na kuwa na hofu ya Mungu.

Katika kituo cha jamii au taasisi inayosaidia watu wenye mahitaji, mtoto anaweza kuona kuwa si kila mtu anakulia katika mazingira yanayofanana.

“Tuwapeleke huko wakaone maisha yalivyo, lakini tusiwafundishe kuwadharau walio katika hali duni. Lengo liwe kumjengea huruma na kutambua kuwa utu haupimwi kwa mali,” anasema Sheikh Mataka.

Sanaa, michezo na mazingira

Kumpeleka mtoto kwenye ukumbi wa sanaa humsaidia kuona ubunifu, muziki, uigizaji na usimulizi wa hadithi kwa vitendo.

Tamasha la utamaduni humfanya aone kuwa utamaduni si jambo la kusoma kwenye kitabu pekee, wakati michezo humfundisha kazi ya pamoja, nidhamu, ushindani na kuheshimu mpinzani.

Aidha, ufukwe, mlima, msitu au hifadhi humsaidia mtoto kuondoka kwenye skrini na kukutana na mazingira ya asili.

Wataalamu wa saikolojia wanaeleza kuwa mazingira hayo yanaweza kuchochea udadisi na ubunifu kwa sababu mtoto hujifunza kupitia kuona, kugusa na kuchunguza.

Chuo kikuu, maeneo ya kihistoria

Mzazi asisubiri mtoto amalize sekondari ndipo aanze kuzungumza naye kuhusu chuo kikuu na taaluma.

Ziara ya chuo kikuu inaweza kumsaidia kuanza kuona uwezekano wa maisha yake ya baadaye na kutambua taaluma mbalimbali.

Vilevile, kumpeleka kwenye eneo la kihistoria na kumsimulia kilichotokea hapo hufanya historia iwe uzoefu halisi.

Makaburi na historia ya familia

Makaburi yanaweza kuwa sehemu ya mazungumzo yanayolingana na umri kuhusu maisha, kifo, kumbukumbu na urithi. Hata hivyo, mazungumzo hayo yasitumike kumtisha mtoto.

Mzazi pia anaweza kumpeleka katika mji alikokulia, nyumbani kwa babu na bibi, biashara ya familia au sehemu ambako wazazi walikulia.

Hii humsaidia mtoto kuelewa kuwa maisha yake ni sehemu ya simulizi kubwa lililotangulia kuzaliwa kwake.

Moja ya safari muhimu zaidi inaweza kuwa kwenda sehemu ambayo mtoto hajawahi kufika. Mji mwingine, mazingira tofauti au jamii yenye utamaduni mwingine vinaweza kumlazimisha kuangalia, kuuliza, kuzoea na kujifunza.

Malezi bora si kumkinga mtoto dhidi ya dunia kila wakati, bali kumtayarisha kuikabili dunia kwa uelewa.

Kabla hajafikisha miaka 13, mtoto anaweza kuwa amejifunza kuhusu fedha, kazi, historia, utamaduni, mazingira, huruma, afya, imani, huduma kwa jamii na thamani ya maisha ikiwa mzazi atampa nafasi ya kujifunza nje ya darasa.

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *