Geita. Kuna miji ambayo huijui mpaka uambiwe, lakini kuna miji ambayo ukifika mara moja, unaelewa kwa nini watu wanaizungumzia. Katoro ni mmoja wapo.
Mwezi uliopita, jina la mji huo lilivuka mipaka ya kawaida ya biashara na uchimbaji dhahabu na kuingia kwenye gumzo la kitaifa baada ya kufanyika kwa sherehe ya kifahari ya kumuaga Monalisa Buyamba, binti wa mfanyabiashara na mchimbaji dhahabu, Sylivester Buyamba, maarufu ‘GSM wa Katoro.’
Helikopta iliyomfuata Monalisa nyumbani na kumpeleka kwenye ukumbi wa sherehe, pamoja na zawadi ya hundi ya Sh1.04 bilioni, vilifanya wengi waliokuwa hawaijui Katoro waanze kujiuliza: Katoro ni mji wa aina gani?
Kwa nini watu wana pesa kiasi hicho? Na ni nini kinachoufanya mji huo uwe na mvuto mkubwa kiasi hiki? Wengine wanaita Kariakoo ya Geita.
Jibu lake halipo kwenye harusi pekee, lipo kwenye dhahabu, samaki, biashara ya jumla, usafirishaji, kilimo, watu wanaohama kutoka maeneo mbalimbali na kasi ya mji unaokua kuliko miundombinu yake.
Kwa mtu ambaye hajawahi kufika Katoro, mji huo unaweza kuonekana kama kituo kingine cha biashara Kanda ya Ziwa. Ukiingia unakuta ni mji wenye mchanganyiko wa shughuli na watu kutoka maeneo mbalimbali.
Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro inaundwa na kata tatu za Nyamigota, Ludete na Katoro. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, maeneo hayo yalikuwa na jumla ya wakazi 231,332.
Hata hivyo, ongezeko la watu kutokana na kuzaliwa na uhamiaji kutoka maeneo mengine limeifanya idadi hiyo kutajwa kuwa imevuka watu 300,000.
Katoro iko takribani kilomita 42 kutoka Geita mjini, safari inayoweza kuchukua dakika 30 hadi 40 kwa mujibu wa hali ya usafiri. Kutoka Mwanza ni karibu kilomita 167, Bukoba kilomita 258, Biharamulo kilomita 92, Chato kilomita 74 na Bukombe kilomita 103.
Uwepo wa Uwanja wa Ndege wa Chato, uliopo takribani kilomita 61 kutoka Katoro, pamoja na Uwanja wa Ndege wa Mwanza, uliopo zaidi ya kilomita 170, nao umeongeza njia za kuufikia mji huo.
Baada ya kuzinduliwa kwa Daraja la JP Magufuli katika eneo la Busisi, usafirishaji kwa barabara umeendelea kupata msukumo zaidi, hasa kwa biashara zinazounganisha Kanda ya Ziwa na maeneo ya Magharibi.
Ukifika Katoro, baadhi ya mitaa utakayosikia ikitajwa mara kwa mara ni California, Kilimanjaro, Stamico, Mji Mwema, Mchongomani, Mtaa wa Afya, Merelani na Kilimahewa. Kinachovutia zaidi si majina ya mitaa pekee, ni kasi ya shughuli zilizopo.
Asubuhi, wafanyabiashara wanafungua maduka. Sokoni, wanawake wanawahi mbogamboga, samaki, ndizi na nafaka. Magari yanaingia na kutoka, pikipiki zinabeba abiria na mizigo, na wafanyabiashara kutoka mikoa jirani wanafika kutafuta bidhaa za jumla.
Katikati ya yote hayo, kuna dhahabu ambayo ni injini kubwa ya uchumi wa eneo hilo. Migodi inayopatikana katika maeneo yanayozunguka Katoro, ikiwamo Msasa, Buckreef, Nyarugusu, Nyaruyeye na Rwamugasa, imekuwa ikichochea mwingiliano wa watu na fedha.
Ndiyo maana Katoro si tu mahali pa kuishi; kwa watu wengi, ni mahali pa kutafuta fursa. Mji huo umejijengea nafasi kama soko la bidhaa za jumla kwa wafanyabiashara kutoka Geita na mikoa jirani, ikiwamo Kagera na Kigoma.
Katika eneo linalotambulika kama Soko la Kariakoo la Katoro, mfanyabiashara anaweza kupata simu, vifaa vya umeme, vifaa vya muziki, vifaa vya ushonaji, vitambaa, nguo na bidhaa nyingine za matumizi.
Kwa upande wa chakula, Soko la Katoro-CCM ndilo moja ya kitovu kikubwa. Huko ndipo bidhaa kama nafaka, ndizi, viazi, mihogo, magimbi, matunda na samaki hupatikana.
Katoro inasifika kwa kuwa na matawi ya benki zaidi ya matano, hali inayofanya uhakika wa usalama kifedha kuwa mkubwa.
Uwepo wa vijiwe vya nyama choma, gym za mazoezi, sauna, supermarket, vimeutofautisha mji huo na maeneo mengine katika ukanda huo. Licha ya makao makuu ya mkoa huo kuwa Geita Mjini, Katoro ndiyo moja ya eneo lenye mwingiliano wa watu na biashara kuliko kwingineko.
Sababu Katoro kuchangamka
Beatrice John, mkazi wa Merelani na mfanyabiashara wa samaki katika Soko la Samaki Katoro-CCM, anasema uchimbaji wa madini una athari ya moja kwa moja kwenye biashara yake.
Anaeleza fedha zinazopatikana migodini huingia kwenye mzunguko wa biashara mjini Katoro na kuufanya mji huo kuchangamka.
“Wachimbaji wanapopata pesa kule, lazima huku Katoro pachangamke, kwa sababu kama samaki unauza Sh8,000, unaweza kumuuzia mteja kwa Sh9,000 au Sh10,000 na hakatai, yeye anafika analipa,” anasema.
David Charles, mkazi wa Katoro anayefanya biashara ya nafaka na samaki kwa zaidi ya miaka 20, anasema samaki ni moja ya biashara zinazozungusha fedha kwa kasi mjini hapo.
Anasema kila asubuhi hupokea magari matatu hadi matano pamoja na zaidi ya pikipiki 100 zinazoleta samaki kutoka maeneo ya ziwani. Kufikia saa tano asubuhi, anasema, mzigo mkubwa huwa tayari umenunuliwa na wafanyabiashara husubiri awamu nyingine inayofika mchana na jioni.
“Biashara ya samaki inalipa kuliko ujasiriamali mwingine ulioko hapa. Hata mwenye duka, mimi ninayefanya ujasiriamali wa samaki, ananifuata mimi, kuna uzalishaji sana kwenye samaki,” anaeleza.
Kwa mtazamo wake, ukiondoa dhahabu yenye thamani kubwa, samaki ni miongoni mwa shughuli zinazoweka fedha kwenye mifuko ya watu wengi kwa wakati mmoja, lakini biashara hiyo ina misimu yake. Kipindi cha kiangazi, upatikanaji wa samaki huwa mgumu zaidi ikilinganishwa na msimu wa masika.
Hata baiskeli inazungusha uchumi wa Katoro
Mkazi wa Rumasa, Matumbate Emmanuel, anaendesha baiskeli ya abiria, maarufu ‘daladala’. Kazi hiyo, anasema, imemsaidia kumudu maisha ya familia yake yenye watoto saba na mke, na kwa siku anaweza kupata kati ya Sh20,000 na Sh25,000.
Mkazi wa Kilimahewa, Abel Kasanda, ni mmoja wa watu ambao hadithi ya Katoro imegusa maisha yao moja kwa moja. Akiuza vyombo vya kupikia kwa miaka mitatu, anasema aliingia kwenye biashara akiwa hana mtaji mkubwa wala mali.
“Nilianza nikiwa mkono mtupu kwenye hii biashara ya umachinga wa vyombo, sikuwa na nyumba wala kiwanja, lakini kwa sasa namshukuru Mungu nimeshanunua kiwanja na kuanza ujenzi, boma lipo, bado kuezeka tu,” anasema.
Kasanda anasema msimu mzuri wa biashara yake ni kiangazi, wakati baadhi ya wateja kutoka nje ya mji wanapokuwa wamevuna na kuuza mazao yao.
Katoro, mji wa wahamiaji na tamaduni tofauti
Katoro si mji wa kabila moja. Wasukuma, Wasumbwa na Wazinza ni miongoni mwa jamii za mwanzo kuishi katika eneo hilo, lakini kadiri biashara, uchimbaji na usafiri vilivyokua, watu kutoka maeneo mbalimbali wameendelea kuingia.
Wachaga, Wajita, Waha, Wakurya, Wahaya na Wajaruwo ni miongoni mwa jamii zinazopatikana kwa wingi.
Hii ndiyo sababu unaweza kuingia kwenye biashara moja ukakutana na mtu kutoka Kagera, mwingine Kigoma, mwingine Mwanza, huku anayekuuzia bidhaa akiwa mwenyeji wa Geita.
Ukuaji wa Katoro hauonekani kwenye maduka pekee, unaonekana pia kwenye huduma za afya.
Inakadiriwa kuwa kati ya watoto 900 na 1,000 huzaliwa kila mwezi, huku Kituo cha Afya Katoro kikitajwa kuhudumia wastani wa wanawake 33 wanaojifungua kwa siku.
Ongezeko hilo la watu limeongeza mahitaji ya huduma za kijamii na kuufanya mji huo uwe na hospitali yenye hadhi ya wilaya iliyopo Mtaa wa Afya, pamoja na kituo cha afya cha Serikali Katoro-CCM na vituo binafsi.
Usalama ulivyofungua biashara
Mji wenye watu wengi na biashara nyingi unahitaji usalama. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, anasema usalama wa Geita umeimarika kutokana na ushiriki wa wananchi kupitia mfumo wa Polisi Jamii.
“Tunazifanyia kazi taarifa kutoka kwa jamii na wahalifu sugu waliokuwa wanasumbua ndani ya mkoa wetu, hatua mbalimbali za kisheria zimechukuliwa na matokeo yake ndiyo haya. Mkoa wa Geita tunaendelea kula bata saa 24, lakini wananchi wanafanya shughuli zao za kiuchumi,” anasema.
Kasi ya ujenzi holela na ongezeko la watu limefanya baadhi ya maeneo ya Katoro kuwa na changamoto ya barabara na mitaro. Baadhi ya barabara huwa ngumu kupitika, huku katika maeneo mengine wananchi wakilalamikiwa kwa kuziba mitaro.
Changamoto hiyo huwa kubwa zaidi wakati wa dharura, hasa pale moto au tukio jingine linapotokea na magari yanahitaji kufika kwa haraka.
Barabara ya Katoro-Bukombe, yenye urefu wa zaidi ya kilomita 58, nayo imekuwa kilio cha wafanyabiashara na wachuuzi.
Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Geita, Hosea Machaka, anasema ujenzi wa barabara hiyo wenye thamani ya Sh10.9 bilioni ulikuwa umefikia asilimia 48 wakati wa taarifa hii.
Kukamilika kwake kunatarajiwa kurahisisha usafirishaji na kuongeza zaidi mwingiliano wa kibiashara kati ya maeneo hayo.


Leave a Reply