Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kutenga mabilioni ya fedha ili kukamilisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, wananchi wameendelea kubeba mzigo wa gharama za matibabu kwa kulazimika kuuza mifugo, mashamba na mali nyingine kugharimia safari, malazi na matibabu nje ya mkoa.
Hali hiyo inatokana na kutokamilika kwa jengo la ghorofa tatu la hospitali hiyo, lililoanza kujengwa mwaka wa fedha 2016/17. Kwa mujibu wa mkataba, mradi huo ulitakiwa kuwa umekamilika Juni 2019.
Mamia ya wagonjwa wanalazimika kufunga safari kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo mkoani Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (Mwanza), Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini-KCMC (Kilimanjaro) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (Dar es Salaam) kufuata huduma za kibingwa.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi, safari hizo za kusaka huduma, malazi na gharama za matibabu zimesababisha baadhi ya familia kuwa maskini na pia kuhatarisha maisha ya wapendwa wao.
Christina Hamis (69), mkazi wa kijiji cha Muhintiri, Ikungi mkoani Singida, anasema alilazimika kuhamia Dodoma, alikopanga chumba kwa zaidi ya miaka miwili tangu mwaka 2024, ili mtoto wake apate huduma ya kusafisha damu (dialisisi).
Anasema aliuza ng’ombe, shamba na kibanda chake ili kugharimia matibabu, usafiri na malazi.
“Niliuza kila nilichokuwa nacho. Mwisho nilishindwa kuendelea na matibabu kwa sababu sikuwa na uwezo tena,” anasimulia.
Anasema iwapo huduma zingepatikana kwa wakati huo, mtoto wake angeweza kugundulika tatizo lake mapema na kupata matibabu kabla hali haijawa mbaya. Kijana wake alifariki dunia Mei 16, 2026, baada ya kuishiwa fedha za dialisisi.
Wakati Hamis akieleza hayo, tayari huduma ya dialisisi imeanza kupatikana katika hospitali hiyo kuanzia Julai 2026.
“Tunateseka sana. Mgonjwa akihitaji daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, figo au uchunguzi wa vipimo vikubwa, mara nyingi tunaambiwa twende Benjamin Mkapa Dodoma, KCMC, Bugando au Muhimbili. Safari ni ndefu na gharama ni kubwa kiasi kwamba baadhi ya wagonjwa wanashindwa hata kufika,” anasema Hamisi Mussa, mkazi wa Manispaa ya Singida.
Kwa upande wake, mkazi wa Ikungi, Anna Mghamba, anasema: “Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ilitakiwa kutupunguzia adha ya kusafiri mikoa mingine, lakini bado wagonjwa wengi wanapewa rufaa. Familia zinauza mifugo na mali nyingine ili kumudu usafiri, malazi na matibabu.”
Kwa mujibu wa mkazi wa Iramba, Paulo Mwalimu, kuna wagonjwa wanaohatarishiwa maisha kwa kusubiri rufaa au fedha za kwenda hospitali nyingine.
“Tunaiomba Serikali ikamilishe miundombinu na kuajiri madaktari bingwa wa kutosha ili wananchi wa Singida wapate huduma karibu na makazi yao badala ya kutumia siku nzima njiani kwenda kutafuta matibabu,” anasema.
Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Yagi Kiaratu, anasema huduma za kibingwa ni changamoto ya muda mrefu na imekuwa mzigo mkubwa kwa wananchi wa Singida na mikoa jirani.
Anasema changamoto hiyo ilichochea juhudi za kuanzishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, huku wazo la ujenzi likiasisiwa mwaka 2015 na Dk Parseko Kone, aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Singida wakati huo.
“Pamoja na kuanza ujenzi wa baadhi ya majengo muhimu, mradi ulipitia vipindi vya kusuasua kabla ya Serikali kuhuisha utekelezaji wake kupitia fedha za mradi wa Uviko-19,” anasema Kiaratu, aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Singida na diwani wa Majengo (2020–2025) kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge.
Kiaratu anasema kuchelewa kukamilika kwa miundombinu hiyo kuliwalazimu wagonjwa wengi kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta huduma katika hospitali za Dodoma, Makiungu, Bugando na Muhimbili, jambo lililowaongezea gharama za matibabu, usafiri na malazi.
Anasema hali hiyo ilikuwa ngumu zaidi kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za mara kwa mara, ikiwamo dialisisi.
Anaeleza kuanza kwa huduma hiyo Singida kumepunguza kwa kiasi kikubwa adha kwa wagonjwa na familia zao.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Dk Munaji Kamtande, anasema licha ya kutokamilika kwa ujenzi wa majengo hayo, hospitali tayari imeongeza huduma za kibingwa, zikiwamo za upasuaji wa mifupa, upasuaji wa ubongo, upasuaji wa mfumo wa mkojo kwa wanaume, maabara za kisasa na CT Scan.
Anasema huduma za dialisisi zimeanza kutolewa Julai 2026, hivyo wagonjwa wengi hawatalazimika kusafiri hadi Dodoma kwa ajili ya matibabu hayo.
Hata hivyo, anakiri kuwa baadhi ya huduma, ikiwamo MRI na matibabu maalumu ya saratani, bado zinahitaji wagonjwa kupewa rufaa kwenda hospitali za juu zaidi.
Anasema kukamilika kwa jengo jipya kutapanua uwezo wa hospitali kutoa huduma zaidi za kibingwa na kupunguza kwa kiasi kikubwa rufaa zinazotolewa nje ya mkoa.
Hospitali hiyo ikikamilika, inatarajiwa kuwa na wodi za watoto, wanawake na magonjwa ya ndani, pamoja na ICU, EMD, vyumba vya upasuaji, maabara za kisasa na huduma nyingine za kibingwa. Huduma hizo zinatarajiwa kupunguza utegemezi wa wakazi wa Kanda ya Kati kwa hospitali za Dodoma, Bugando na Muhimbili.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Jessica Lebba, anasema ujenzi umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha serikalini.
Anasema mradi kwa sasa unatekelezwa katika awamu ya tatu, huku uongozi wa mkoa na hospitali ukiendelea kufuatilia maendeleo yake ili kuhakikisha unakamilika kwa ubora unaotakiwa.
“Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha kwa kiasi kikubwa huduma za kibingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida na kupunguza rufaa zinazotolewa sasa kwenda hospitali nyingine,” anasema.
Dk Lebba anasema kwa sasa hospitali inatoa zaidi ya huduma 10 za kibingwa, lakini baada ya jengo kukamilika, inatarajiwa kufikia lengo la kutoa huduma zote 17 za kibingwa na kuwa kituo kikubwa cha utoaji wa huduma hizo kwa wakazi wa Kanda ya Kati.
Athari za ucheleweshaji wa miradi
Daktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji, Mugisha Nkoronko, anasema huduma za afya zinapokuwa mbali na wananchi huleta adha na gharama kubwa, huku baadhi ya wagonjwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu ambayo wangepaswa kuyapata karibu na maeneo wanayoishi.
Vilevile, anasema huongeza hatari kwa wagonjwa, hasa wanaohitaji huduma za haraka na za kibingwa.
Dk Nkoronko anasema uwekezaji katika vituo vya afya ni jambo muhimu kwa sababu unasaidia kupunguza umbali ambao wananchi hulazimika kusafiri wanapohitaji huduma.
Anasema uwekezaji haupaswi kuishia kwenye ujenzi wa majengo pekee, bali unatakiwa kwenda sambamba na upatikanaji wa vifaa tiba na rasilimali watu wa kutosha katika maeneo ambako wananchi wanapatikana.
Ni mtazamo wake kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inapaswa kuimarishwa ili kutoa huduma zinazohitajika na kupunguza mzigo wa wagonjwa wanaolazimika kwenda mikoa mingine kupata huduma za kibingwa.



Leave a Reply