Skip to content
-
Subscribe to our newsletter & never miss our best posts. Subscribe Now!
  • https://www.facebook.com/
  • https://twitter.com/
  • https://t.me/
  • https://www.instagram.com/
  • https://youtube.com/
Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

Habarimpya

Habari Mpya Kilasiku

  • Home
  • Sample Page
  • Home
  • Sample Page
Subscribe
Close

Search

Habari

MUHAS yaanzisha tiba ya kibingwa ya kinywa, meno kwa watoto

By admin
August 17, 2026 3 Min Read
0

Dar es Salaam. Watoto wenye matatizo ya meno nchini wameanza kupata huduma kutoka kwa madaktari bingwa baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kuanzisha kituo maalumu cha huduma za afya ya kinywa na meno kwa watoto.

Kituo hicho, kilicho chini ya Shule Kuu ya Afya ya Kinywa na Meno, ni cha kwanza nchini kutoa huduma maalumu kwa watoto na tayari kimeanza kutoa huduma kwa majaribio tangu Mei mwaka huu.

Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa, akizungumza leo Jumatatu, Agosti 17, 2026, jijini Dar es Salaam, amesema watoto 27 wamepatiwa matibabu tangu huduma hiyo ilipoanza.



Amesema miongoni mwa matatizo yanayowakabili watoto ni kuoza kwa meno, meno kupishana, saratani na changamoto nyingine za afya ya kinywa ambazo sasa zitaweza kushughulikiwa na madaktari bingwa.

Profesa Kamuhabwa amesema kuanzishwa kwa kituo hicho ni sehemu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki kupitia Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TİKA) na Chuo Kikuu cha Ankara.

“Tuna kitengo cha upasuaji ambapo mtoto huletwa, hufanyiwa uchunguzi na, inapobidi, hupatiwa matibabu chini ya dawa za usingizi. Huduma hii ni muhimu kwa sababu wapo watoto wenye mahitaji maalumu, wakiwamo wenye mtindio wa ubongo, ambao awali ilikuwa vigumu kuwahudumia,” amesema.

Amesema utaratibu huo pia unawasaidia watoto wanaoogopa sindano, kwa kuwa wanaweza kupewa dawa za usingizi wakati wa matibabu badala ya kutegemea njia za kawaida za ganzi.

Katika ushirikiano huo, amesema madaktari bingwa wa kinywa na meno, wataalamu wa usingizi, wauguzi na wataalamu wa maabara wamepata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Ankara.

Takwimu za Wizara ya Afya za mwaka 2025 zinaonesha asilimia 76.5 ya Watanzania wenye umri wa miaka 15 na zaidi wamewahi kuathiriwa na kuoza kwa meno, huku asilimia 31.1 ya watoto wakiwa na tatizo la kuoza meno ya utotoni.

Aidha, asilimia 68 ya watu wazima nchini wanakabiliwa na magonjwa ya fizi, huku tatizo hilo likiwakabili asilimia 57 ya watoto.

Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa takriban asilimia 31 ya watoto wana changamoto ya mpangilio usio sahihi wa meno.

Mafunzo ya huduma za dharura

Profesa Kamuhabwa amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki hauishii katika huduma za meno kwa watoto, bali pia unahusisha kuimarisha huduma za dharura.

Amesema MUHAS imepokea gari maalumu kwa ajili ya mafunzo ya huduma za dharura na imeanza mpango wa kuwajengea uwezo watu ambao si madaktari ili waweze kutoa huduma za awali wakati wa dharura.

Amesema mpango huo ni sehemu ya maandalizi ya kuimarisha huduma za afya kuelekea Michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027, ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza pamoja na Kenya na Uganda.

“Wakati wa dharura, mtu anaweza kupoteza maisha kutokana na kuhudumiwa vibaya. Wakati mwingine watu humshika mgonjwa au kumbania hewa bila kujua namna sahihi ya kumsaidia. Ndiyo maana katika ushirikiano huu tumekubaliana kuongeza uwezo wa wataalamu katika huduma za dharura,” amesema.

Amesema maandalizi ya mashindano makubwa yanahitaji wataalamu wa kutosha, pamoja na watu wenye ujuzi wa kutoa huduma za awali za dharura.

Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dk Bekir Gezer, amesema kuanzishwa kwa huduma hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo katika sekta ya afya.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa TİKA, Halim Omer, amesema ushirikiano na MUHAS utajikita katika kujenga uwezo wa wataalamu, kufanya tafiti, usomaji wa picha za kitabibu kwa kutumia akili bandia na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya matibabu.

Kwa mujibu wa MUHAS, ushirikiano huo pia umehusisha uboreshaji wa miundombinu ya Shule ya Meno na mafunzo ya wataalamu katika Chuo Kikuu cha Ankara.

Author

admin

Follow Me
Other Articles
Previous

Wakurugenzi wa Halmashauri wabebeshwa zigo la mazingira

Next

Nishati mbadala yatajwa kuwa suluhu ya uharibifu wa mazingira

No Comment! Be the first one.

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recent Posts

  • VETA YAANDAA MTAALA WA MAFUNZO YA MUDA MFUPI WA FANI YA RECYCLING
  • VETA IMETAKIWA KUENDELEA KUWASHIRIKISHA WATAALAMU WALIOBOBEA FANI MBALIMBALI
  • BAHI IMETENGA MILLION 100 KUTOKA MAPATO YAKE YA NDANI KUSAIDIA VIJANA WA WILAYA KUPATA ELIMU VETA
  • *WAKULIMA WA KITOMONDO WANUFAIKA NA HUDUMA YA MAWASILIANO*
  • MAGAZETINI LEO JUMATATU AGOSTI 17/2026

Recent Comments

  1. A WordPress Commenter on Hello world!

Archives

  • August 2026

Categories

  • Habari
Copyright 2026 — Habarimpya. All rights reserved. Blogsy WordPress Theme