Rais Mwinyi: Zanzibar Yafungua Fursa Mpya za Ushirikiano na Urusi

Global Publishers
September 28, 2026
18 views
0 Comments

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar iko tayari kuimarisha ushirikiano na Shirikisho la Urusi katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo leo, Septemba 28, 2026, alipokutana na ujumbe kutoka Shirikisho la Urusi ulioongozwa na Denis Agafonov, Mkuu wa Kurugenzi ya Wataalamu katika Ofisi ya Rais wa Shirikisho la Urusi, katika Ikulu ya Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Mwinyi amesema Zanzibar inalenga kutumia fursa za ushirikiano na Urusi katika maeneo ya nishati, bandari na usafirishaji, utalii, elimu na utafiti, afya, uvuvi pamoja na Uchumi wa Buluu.

Amesema ushirikiano huo unaweza pia kufungua fursa zaidi katika uwekezaji na matumizi ya teknolojia, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha maeneo yanayojadiliwa yanabadilishwa kuwa miradi yenye matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Rais Mwinyi amesema Zanzibar iko tayari kushirikiana na Urusi katika tafiti za pamoja na kuendeleza sekta ya Uchumi wa Buluu, ambayo ni miongoni mwa maeneo muhimu katika ajenda ya maendeleo ya Zanzibar.

Kwa upande wake, Denis Agafonov amesema Urusi iko tayari kuendelea na mazungumzo na Zanzibar kuhusu maeneo yenye fursa za ushirikiano na uwekezaji.

Mazungumzo hayo yanaongeza wigo wa fursa za ushirikiano kati ya Zanzibar na Urusi katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.