FAIDA KUU YA LISHE BORA

 

 

NA BIBI MAENDELEO IRENE SAMORA

Lishe bora ni msingi muhimu katika ukuaji, afya na maendeleo ya mtoto, huku jamii ikihimizwa kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili wenye virutubisho muhimu kwa ajili ya kuimarisha afya ya mwili na akili.

Akizungumza katika kipindi cha Bibi Maendeleo, kinachorushwa na Matukio Daima TV, Bibi Maendeleo Irene Samora amesema jamii inapaswa kuwa na uelewa mpana kuhusu umuhimu wa lishe bora, hususan kwa watoto, ili kusaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na ukosefu wa lishe sahihi.

Irene amesema watoto wanapaswa kula mlo wenye mchanganyiko wa vyakula kutoka katika makundi mbalimbali, ili miili yao iweze kupata virutubisho vinavyohitajika kwa ajili ya ukuaji na maendeleo.

Amesema mlo bora unapaswa kuzingatia makundi mbalimbali ya vyakula, ikiwemo vyakula vya wanga, protini, mboga za majani na mboga nyingine, matunda pamoja na mafuta kwa kiasi kinachofaa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa virutubisho kama vitamini A, vitamini C na madini ya zinki, ambavyo vina mchango muhimu katika kuimarisha afya na kinga ya mwili. Virutubisho hivyo vinaweza kupatikana kupitia ulaji wa vyakula mbalimbali, ikiwemo matunda na mboga.

Kwa upande wa wazazi na walezi, Irene amewataka kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili na wenye mchanganyiko wa vyakula, huku wakizingatia pia usafi na usalama wa chakula kinachotayarishwa na kutolewa kwa watoto.

Ameongeza kuwa maziwa ya mama yana umuhimu mkubwa kwa mtoto, hasa katika hatua za mwanzo za maisha, kutokana na kuwa chanzo muhimu cha virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji na kinga ya mtoto.

Katika hatua nyingine, amesema ulaji wa lishe bora unahitaji pia matumizi yenye kiasi ya mafuta, chumvi na sukari, huku wazazi wakitakiwa kudhibiti matumizi ya vyakula vyenye chumvi na sukari nyingi.

Aidha, watoto wanapaswa kupewa maji ya kutosha na kuhamasishwa kula matunda pamoja na mboga mbalimbali ili kupata vitamini na madini muhimu kwa afya ya mwili.

Irene amesisitiza pia umuhimu wa wazazi na walezi kufuatilia ukuaji na maendeleo ya watoto, kuhakikisha wanapata chakula chenye virutubisho mbalimbali na kuzingatia usafi katika maandalizi, uhifadhi na utoaji wa chakula.TAZAMA KIPINDI HAPA

Amesema jamii ikiwa na uelewa sahihi kuhusu lishe na kuwajibika katika kuhakikisha watoto wanapata chakula bora, itaweza kuchangia katika kupunguza changamoto za utapiamlo na kuwezesha watoto kukua wakiwa na afya bora.

Bibi Maendeleo Irene Samora ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuendelea kuipa kipaumbele lishe ya watoto, kwa kuwa mtoto mwenye lishe bora ana nafasi kubwa ya kukua, kujifunza na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku.