
ARUSHA: Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ametoa wito kwa viongozi wa taasisi za umma kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na badala yake kuelekeza fedha katika kuwawezesha vijana kwa kuwajengea uwezo na uzoefu.
Ndejembi ameyasema hayo leo Septemba 28, 2026, katika hafla ya kufungua Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs FORUM 2026) iliyofanyika katika ukumbi wa AICC, jijini Arusha.
Amesema kuwa viongozi wa taasisi na mashirika ya umma wana wajibu wa kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na kuelekezwa katika shughuli zenye manufaa kwa wananchi, hususan kuwawezesha vijana kupata ujuzi na uzoefu utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.
