Sifa Gospel Fest 2026: Suma Awaunganisha Vijana na Fursa za Maisha – Video

MWANZA — Mratibu Mkuu wa ibada ya kusifu na kuabudu ya Sifa Gospel Fest 2026, Suma Mwaitenda, amewataka vijana kufikiri nje ya boksi na kutambua uwezo na ujuzi walionao ambao unaweza kuwaongezea thamani katika maisha, mbali na vyeti vya taaluma walivyopata shuleni.

Suma ameyasema hayo jijini Mwanza wakati wa mafunzo katika kliniki ya vijana iliyopewa jina la Sifa Youth Talk, iliyofanyika kwa mara ya kwanza kwa lengo la kuongeza thamani katika maisha ya vijana kupitia elimu kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo maadili, uchumi na jamii.

Akizungumza kuhusu Career Development, yaani ukuzaji wa safari ya kitaaluma na kikazi, Suma amesema vijana wanapaswa kutambua ujuzi wao na namna wanavyoweza kuutumia katika kujenga maisha yao.

“Nje ya vyeti, una ujuzi gani unaouzika? Haijalishi umesoma nini.”



Aidha, leo inafanyika siku ya kilele cha ibada kubwa ya kusifu na kuabudu ya Sifa Gospel Fest 2026, inayofanyika katika Uwanja wa Furahisha, Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

Akizungumzia maandalizi ya ibada hiyo, Suma amesema maandalizi yote yamekamilika huku akieleza kuwa mwitikio kutoka kwa wakazi wa Mwanza umekuwa mkubwa.

“Maandalizi yote ya ibada hii yamekamilika, mwitikio wa watu wa Mwanza ni mkubwa na tumebarikiwa kuwa na listi kubwa ya watumishi wa Mungu na waimbaji ambao watahudumu leo,” amesema.

Suma amesema ibada hiyo imeendelea kuwagusa watu mbalimbali, huku akieleza kuwa waandaaji wanaamini kuwa kupitia kusifu na kuabudu, watu wanaweza kupata uponyaji.

“Ibada hii imeendelea kuwagusa watu wengi ambao, na sisi tunaamini kuwa katika kusifu kuna uponaji na watu wengi wameendelea kupona kupitia ibada hii,” amesema.

Katika hatua nyingine, wasanii mbalimbali wanaotarajiwa kuhudumu katika ibada hiyo wameeleza furaha yao kwa tukio hilo kufika jijini Mwanza, huku wakitoa shukrani kwa waandaaji kwa nafasi ya kushiriki katika Sifa Gospel Fest 2026.