CCM Iringa yamkabidhi Asas tuzo ya heshima – HabariLeo

IRINGA: KATIBU wa NEC Idara ya Oganaizesheni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Matiko Chacha (MCC), amemkabidhi Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Salim Abri Asas, tuzo maalumu ya heshima iliyotolewa na CCM Mkoa wa Iringa kwa kutambua mchango wake katika ujenzi na uimarishaji wa Chama.

Tuzo hiyo imetolewa baada ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa kuwasilisha hoja ya kumtambua Asas, ambayo ilipitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Mkoa wa Iringa uliofanyika katika Chuo cha UVCCM Ihemi.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Asas amesema viongozi wa sasa wanapaswa kufanya mambo yatakayobaki kuwa kumbukumbu ndani ya CCM, akisema kizazi kijacho kitakuja kuwauliza walifanya nini walipokuwa na dhamana ya uongozi.

“Kizazi kitakuja kutuuliza, mlilikifanyia nini CCM?” amesema Asas aliyekuwa akishangiliwa kwa nguvu na wajumbe wa Mkutano huo.

Amesema swali hilo limekuwa sehemu ya msukumo wake wa kushiriki katika ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya Chama, hususan ujenzi wa ofisi za CCM katika ngazi ya Kata.

Asas amesema ni jambo lisilofaa kwa CCM kufikisha miaka 50 huku baadhi ya Kata zikiwa hazina ofisi za Chama, miradi au makazi kwa ajili ya watumishi wake.

Amesema kutokana na msimamo huo, amejitolea kuhakikisha ifikapo CCM inatimiza miaka 50, kila Kata inakuwa na ofisi ya Chama, akieleza kuwa baadhi ya miradi hiyo tayari imekamilika huku mingine ikiendelea.

“Tumejiwekea msimamo kwamba itakuwa aibu kufikia miaka 50 ya CCM, halafu kuna Kata ambazo hazina ofisi za Chama,” amesema.

Amesema dhamira yake ya kuona ofisi hizo zinakamilika imefikia hatua ya kuiweka kazi hiyo kwenye wosia wake kwa wanafamilia, akieleza kuwa amewaeleza ndugu zake kwamba iwapo Mungu atamchukua kabla ya kukamilisha azma hiyo, wahakikishe fedha zinatengwa kutoka kwenye mali ya familia ili kukamilisha ujenzi wa ofisi hizo.

Kwa mujibu wa Asas, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kazi aliyoianza inaendelea hata kama hatakuwepo, ili ofisi hizo zitumike na viongozi na wanachama wa CCM wa sasa na vizazi vijavyo.

Amesema anataka mchango wake ndani ya Chama usibaki kwenye maneno pekee, bali uonekane kupitia miradi na miundombinu itakayodumu na kuwa na manufaa kwa wanachama kwa muda mrefu.

Akimpongeza Asas kwa tuzo hiyo, Chacha, amewataka viongozi na wanachama kuendelea kujipanga na kuweka mikakati ya muda mrefu kuelekea miaka 50 ya chama hicho.

Chacha amesema CCM ilipoanzishwa iliweka malengo mbalimbali, likiwemo lengo la kushika dola, hivyo wanachama wanapaswa kuendelea kutafakari namna ya kukiendeleza chama hicho katika vipindi vijavyo.

“Ni muhimu kwa viongozi wa sasa kuacha msingi ambao utakuwa na manufaa kwa vizazi vitakavyokuja na kuhakikisha chama kinaendelea kuwa na mipango madhubuti na muda mrefu,” alisema.

Aidha, amewataka wanachama kuendelea kujiandaa kwa uchaguzi wa chama unaokuja na kuhakikisha wanashiriki katika shughuli za chama kwa umoja na mshikamano.