WASHINGTON: Rais wa Marekani Donald Trump amekataa pendekezo la Iran la kufungua tena Mlango wa Hormuz na kusitisha mapigano yanayoendelea katika Mashariki ya Kati.
Iran iliwasilisha mpango huo wakati wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, ikisema pendekezo hilo lilifikishwa kwa Marekani kupitia wapatanishi kutoka Qatar.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, makubaliano hayo yangeweza kuwezesha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz ndani ya siku saba, sambamba na kusitishwa kwa mapigano katika eneo hilo.
Hata hivyo, Trump amekataa mpango huo akisema Iran inataka kufunguliwa kwa haraka kwa njia hiyo kutokana na shinikizo la kiuchumi linaloikabili.
Trump alisema Iran imeathirika kwa sababu ya kupungua kwa shughuli za usafirishaji kupitia Hormuz, ambayo ni moja ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa nishati duniani.
“Nimekataa pendekezo lao,” Trump aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya White House kabla ya kuondoka kuelekea Tennessee.
Mlango wa Hormuz unaunganisha Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman na una umuhimu mkubwa katika biashara ya kimataifa, hasa kwa usafirishaji wa mafuta na bidhaa nyingine za nishati.
Marekani imeendelea kuweka shinikizo la kiuchumi dhidi ya Iran huku ikitaka Tehran kuondoa vizuizi katika Mlango wa Hormuz.
Iran yaweka wazi msimamo wake
Kwa upande wa Iran, Araqchi amesema Tehran iko tayari kufikia makubaliano iwapo Marekani itaonyesha utayari wa kufanya hivyo.
Alisema pendekezo hilo lingeanza kwa kufunguliwa kwa Hormuz ndani ya muda wa siku saba na kusitishwa kwa mapigano, kabla ya kuanza kwa mazungumzo mapana zaidi kati ya pande zinazohusika.
Mazungumzo hayo yanaweza pia kugusa suala la mpango wa nyuklia wa Iran.
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia na masuala mengine, lakini haitakubali kile alichokiita vitisho, shinikizo au kulazimishwa.
Iran imekuwa ikisisitiza kuwa haitafuti vita, lakini itaendelea kujilinda dhidi ya mashambulizi na vitisho.
Mzozo kati ya Iran, Marekani na Israel umeendelea tangu Februari 28, kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Tangu wakati huo, mapigano yamekuwa yakibadilika kati ya vipindi vya kusitisha mashambulizi na kurejea kwa mapigano, huku kukiwa na madhara kwa miundombinu na uchumi wa Iran.
Iran na washirika wake nao wamejibu kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo mbalimbali katika Mashariki ya Kati.
Kwa sasa, kukataliwa kwa pendekezo la Iran na Trump kunaacha hatma ya kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz ikiwa haijulikani, huku juhudi za kidiplomasia za kusitisha mapigano zikiendelea kufuatiliwa kwa karibu.

