Leo ni Siku ya Vita Uwanjani: Vigogo wa Ulaya na Afrika Kwenye Kivumbi

Viwanja mbalimbali kuwaka moto leo kuanzia hapa Afrika mpaka Kule Ulaya kuhudia mechi za Kimataifa yaani Afcon na Uefa Nations Leagu. Je nani kuibuka mbabe?

Michuano ya UEFA Nations League inaendelea na Czechia atakiwasha dhidi ya  Croatia katika dimba la Fortuna Arena mjini Prague ambapo huu ni moja ya mchezo ambapo utatazamwa sana.

Lakini Czechia wao wana faida zaidi kwani watakuwa nyumbani hivyo uwepo wa mashabiki zao unawapa hamasa ya kupambana zaidi, lakini wanaenda kukutana na Croatia ambayo ina uzoefu mkubwa kwenye mechi kubwa za Kimataifa.

Jambo muhimu kwa Czechia litakuwa kutokaa nyuma kupita kiasi. Timu hiyo ikiwa itapewa muda wa kumiliki mpira, inaweza kuanza kuzungusha mpira hadi ipate nafasi ya kupenya.

Croatia ina kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu na kizazi kipya. Luka Modric na Mateo Kovacic bado ni muhimu kwenye kiungo, huku Joško Gvardiol, Martin Baturina, Petar Sucic na Andrej Kramarić wakiongeza ubora katika maeneo mengine. Kikosi rasmi cha Croatia kinajumuisha pia Perisic, Budimir na Musa.

Mechi kali na ya kibabe ambayo itakuwa inasubiriwa itakuwa ni hii ya Uingereza ambao watakuwa wenyeji wa Hispania kwenye uwanja wa Wembley. Hispania wanaingia kama mabingwa wapya wa dunia wakati vijana wa Thomas wakiazamiwa kufanya vyema kwenye mchezo huu.

Kwa Uingereza, hii ni nafasi kubwa ya kuonyesha kama wamepunguza pengo dhidi ya timu bora za Ulaya. Thomas Tuchel ameuita mchezo huu mwanzo mpya, na kikosi kina vipaji vingi katika maeneo ya kiungo na ushambuliaji.

Hata hivyo, The Lions watakuwa na changamoto kubwa kutokana na kukosekana kwa Declan Rice, Cole Palmer, Marcus Rashford, Tino Livramento na Kobbie Mainoo kutokana na majeraha.

Faida yao kubwa ni kuchezea Wembley. Kucheza mbele ya mashabiki wao kunaweza kuwapa nguvu hasa katika mwanzo wa mchezo.

Hispania wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na kujiamini zaidi baada ya kushinda Kombe la Dunia 2026, sasa wanataka kuendeleza utawala wao kwenye Nations League.

Nguvu yao kubwa ni umiliki wa mpira na uwezo wa kuzungusha mpira kwa kasi, huku wakitumia wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza katika maeneo madogo.

Macho yataelekezwa kwa Lamine Yamal, ambaye anaweza kuwa tatizo kubwa kwa upande wa kushoto wa ulinzi wa Uingereza. Hispania pia wana uwezo wa kubadilisha kasi ya mchezo ghafla kutoka possession ya taratibu kwenda mashambulizi ya haraka.

Kule AFCON pia kuna mechi za pesa lakini tutajikita kwenye mechi ya Afrika Kusini dhidi ya Guinea mchezo wa Kundi D wa kufuzu michuano hii mikubwa Afrika. Mchezo huu una umuhimu mkubwa kwa sababu Kenya, ambayo ipo kwenye kundi hilo, tayari imepata tiketi ya AFCON kama mwenyeji hivyo Afrika Kusini, Guinea na Eritrea zinapigania nafasi iliyobaki.

Ni mchezo wa kwanza wa ushindani kwa Pitso Mosimane tangu arejee kwenye benchi la Bafana Bafana kwa mara ya tatu. Hivyo, kuna presha ya kuanza vizuri, hasa kwa kucheza nyumbani.

Afrika Kusini ina mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu kutoka Mamelodi Sundowns na Orlando Pirates, jambo ambalo Mosimane amelitaja kama moja ya nguvu za kikosi chake. Pia, Bafana wana nafasi nzuri ya kutumia kasi ya wachezaji wao wa pembeni na uwezo wa kutawala mpira katikati ya uwanja.

Lakini kwa upande wa Guinea si timu rahisi. Ingawa iko chini ya Afrika Kusini kwenye viwango vya FIFA, imekuwa mpinzani mgumu katika mikutano yao iliyopita. Rekodi ya hivi karibuni inaonyesha Afrika Kusini ina ushindi mmoja dhidi ya Guinea na sare moja katika mechi mbili zilizopita.

Nguvu kubwa ya Guinea inaweza kuwa kwenye mipira ya juu na nguvu za mshambuliaji Serhou Guirassy, ambaye Mosimane amemtaja kama tishio kubwa kutokana na uwezo wake wa kucheza kama namba tisa na kutumia mipira ya juu.

Mechi ya mwisho kukutana Afrika Kusini waliondoka na ushindi, hivyo hii ni nafasi ya Guinea kulipa kisasi. Je wataweza huku nafasi ya kuondoka na ushindi ikiwa kwenye timu ambayo imejiandaa.