Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetoa taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya wasanii na waandaaji wa shughuli za sanaa baada ya kubainika kuwa wamekiuka maadili na taratibu zinazohusiana na shughuli za sanaa nchini.
1. HARMONIZE AADHIBIWA KWA VIDEO YA “KUDOS”
Msanii Rajab Abdulkahali maarufu Harmonize ameadhibiwa kwa kutenda kosa la kimaadili la kusambaza video ya wimbo unaoitwa “Kudos”, ambayo kwa mujibu wa BASATA haizingatii kabisa maadili ya Kitanzania na inavunja heshima ya misikilizaji au mtazamaji.
BASATA imesema kosa hilo ni kinyume na Kanuni ya 20(a) ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, Tangazo la Serikali Na. 137 la tarehe 22 Mei 2026.

Hadi wakati wa kutolewa kwa taarifa hiyo, BASATA haikupokea utetezi wala maelezo mbadala kutoka kwa Harmonize.
Kwa kuzingatia Kanuni ya 45 ya Kanuni za Baraza, Harmonize amepewa adhabu zifuatazo:
- Kusitisha video ya wimbo “Kudos” kwenye mitandao yake ya kijamii.
- Kulipa faini ya Shilingi milioni tano (TSh 5,000,000) ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi.
- Kutokujishughulisha na kazi za sanaa kwa namna yoyote kuanzia tarehe ya uamuzi hadi atakapotekeleza maamuzi yaliyotolewa.
2. KENNEDY DAVID SANGA
Mwongoza video ya wimbo “Kudos”, Kennedy David Sanga, pia ameadhibiwa baada ya kubainika kuwa alitenda kosa la kimaadili linalokiuka heshima ya misikilizaji au mtazamaji.
Kwa mujibu wa BASATA, Sanga alikiuka Kanuni ya 20(a) ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, Tangazo la Serikali Na. 137 la tarehe 22 Mei 2026, kwa kuongoza video hiyo iliyokuwa na maadili yasiyozingatia maadili ya Mtanzania.
Baada ya kusikilizwa, ilibainika kuwa alitenda kosa hilo na kupewa adhabu zifuatazo:
- Kusitisha video ya wimbo “Kudos” kwenye mitandao yake ya kijamii.
- Kulipa faini ya Shilingi milioni tano (TSh 5,000,000) ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi.
- Kutokujishughulisha na kazi za sanaa kwa namna yoyote kuanzia tarehe ya uamuzi hadi atakapotekeleza maamuzi yaliyotolewa.
3. AVIL CONTRACTORS COMPANY LTD
Avil Contractors Company Ltd, mwandaaji wa shindano la Miss Grand Tanzania, ameadhibiwa kwa kutenda kosa la kuendesha shindano hilo bila kuwa na KIBALI CHA TUKIO kutoka BASATA.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kampuni hiyo ilikiuka Kanuni na taratibu za uendeshaji wa matukio ya sanaa hapa nchini.
BASATA ilisema kampuni hiyo ilipewa notisi ya kosa hilo tarehe 12 Agosti 2026 na kutakiwa kuwasilisha utetezi ndani ya siku 21, lakini haikutekeleza.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 45 ya Kanuni za Baraza, kampuni hiyo imeamriwa:
- Kulipa faini ya Shilingi milioni tatu (TSh 3,000,000) ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi.
- Kutokujishughulisha na kazi za sanaa kuanzia tarehe ya uamuzi hadi itakapotekeleza maamuzi yaliyotolewa.
4. NANDY AADHIBIWA KWA VIDEO YA KIMAAADILI
Msanii Faustina Charles Mfinanga maarufu Nandy ameadhibiwa na BASATA baada ya kutenda kosa la kimaadili la kuvaa nguo isiyokuwa na staha inayovunja heshima ya mtazamaji.
BASATA imesema kosa hilo lilitokea wakati Nandy akitumbuiza katika fainali ya shindano la Miss Universe 2026, lililofanyika katika ukumbi wa Haddypo, kinyume na Kanuni ya 20(a) ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, Tangazo la Serikali Na. 137 la tarehe 22 Mei 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Nandy amekiri kosa, ameshusha video hiyo isiyozingatia maadili ya Mtanzania kwenye mitandao yake ya kijamii na amelipa faini ya Shilingi milioni tatu (TSh 3,000,000).
Hata hivyo, msanii huyo ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake za sanaa chini ya uangalizi.
5. MILLEN PRIVE & CO. LIFESTYLE LIMITED
Millen Prive & Co. Lifestyle Limited, mwandaaji wa shindano la Miss Universe Tanzania, ameadhibiwa kwa kosa la kimaadili lililohusisha msanii Faustina Charles Mfinanga maarufu Nandy.
Kwa mujibu wa BASATA, kampuni hiyo ilitenda kosa la kuvaa nguo ambayo haina staha inayovunja heshima ya mtazamaji, wakati Nandy akitumbuiza kwenye fainali ya Miss Universe Tanzania 2026 iliyofanyika katika ukumbi wa Haddypo, Dar es Salaam.
BASATA imesema kosa hilo ni kinyume na Kanuni ya 20(2)(a) ya Kanuni za Baraza la Sanaa la Taifa, Tangazo la Serikali Na. 137 la tarehe 22 Mei 2026.
Baada ya kusikilizwa, ilibainika kuwa kampuni hiyo ilitenda kosa la kimaadili na imepewa adhabu zifuatazo:
- Kulipa faini ya Shilingi milioni tatu (TSh 3,000,000) ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi.
- Kupewa onyo kali na kutakiwa kuwa makini wakati wa kutekeleza kazi zake za sanaa.
BASATA imetoa rai kwa wasanii na wadau wa sanaa kuhakikisha wanazingatia Sheria, Kanuni, Miiongozo na Maadili ya Mtanzania wanapotekeleza kazi zao za sanaa.



