Wadau kujadili maendeleo ya kidijitali, data ikipewa kipaumbele
Zanzibar. Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa tamasha la data Africa 2026, tukio litakalowakutanisha zaidi ya washiriki 300, mashirika zaidi ya 100, kutoka nchi 30 litakalofanyika katika Hoteli ya Verde, Zanzibar.
Tamasha hilo litakalofanyika siku tatu limeandaliwa kwa ushirikiano wa Tanzania Data Lab (dLab) na Pollicy Uganda, ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa karibu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu ya Zanzibar.
Linatarajia kuonyesha namna taasisi, wabunifu na jamii za Afrika zinavyovuka hatua ya mijadala na kuanza kujenga suluhisho halisi kwa kutumia data, teknolojia za kidijitali na Akili Unde (AI).
Akizungumza kuhusu tamasha hilo leo Agosti 18, 2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Data Lab, Dk Mahadia Tunga amewahimiza wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi na kwa fahari katika tukio hilo.
“Data inasaidia kubaini vipaumbele vya maendeleo na kuhakikisha kuwa rasilimali zetu chache zinatumiwa kwa ufanisi barani kote. Data Tamasha Africa ni jukwaa kuu la kukutana, kujifunza kutoka kwa wale waliofanikiwa, na kujadili kwa uwazi changamoto tunazoshirikiana kwa sababu hakuna mafanikio yanayokuja bila vikwazo,” amesema Dk Mahadia.
Kwenye tamasha hilo lenye kauli mbinu isemayo: “Kujenga na Data / Building with Data,” washiriki wataonesha suluhisho za Akili Unde (AI) zilizobuniwa Afrika, mifumo ya data inayotokana na mahitaji ya jamii, ubunifu katika huduma za kidijitali na teknolojia zinazolenga kutatua changamoto halisi za maendeleo barani Afrika.
Tamasha hilo litawakutanisha wanasayansi wa data, watunga sera, watafiti, wabunifu, washirika wa maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia, vijana na wabunifu wa sanaa.
Pia litatoa nafasi ya kujifunza, kushirikiana na kuanzisha ushirikiano mpya.
Kwa Zanzibar, kuwa mwenyeji wa Data Tamasha Africa 2026 kunaimarisha nafasi yake kama kitovu kinachokua cha ubunifu wa kidijitali, maendeleo yanayoongozwa na data na utawala wa kidijitali Afrika Mashariki.
Naye Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uvumbuzi, Mudrik Ramadhan Soraga amesema Zanzibar imejipanga kikamilifu kuwa mwenyeji wa tukio hilo.
Pia amesema kuandaa jukwaa hilo kutainua hadhi ya Zanzibar kimataifa kama kitovu cha uvumbuzi wa kidijitali, huku likiwavutia wawekezaji katika Tehama, elimu, biashara na huduma za jamii.
“Tunataka kuona data na teknolojia zikitumika kama zana za kuongeza tija, uwajibikaji na maendeleo endelevu,” amesema Soraga.
