Makosa matatu yasababisha daladala 203 kufungiwa VTS
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imeanza kufunga vifaa vya kufuatilia mwenendo wa magari (VTS) katika daladala zinazofanya safari za mijini, hatua inayolenga kudhibiti ukiukwaji wa masharti ya leseni na kuboresha huduma kwa abiria.
Hadi Agosti 12, 2026, jumla ya daladala 203 jijini Dar es Salaam zilikuwa zimefungiwa vifaa hivyo kutokana na ukiukwaji wa masharti ya uendeshaji, huku gharama za ufungaji zikibebwa na wamiliki wa magari husika.
Akizungumza na Mwananchi Agosti 13, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Latra, Salum Pazzy, amesema hatua hiyo imeanza Dar es Salaam kutokana na ukubwa wa changamoto za usafiri wa daladala katika jiji hilo.
Amesema makosa yanayoongoza katika hatua hiyo ni upandishaji wa nauli kinyume cha viwango vilivyowekwa, kukatisha safari kabla ya kufika mwisho wa ruti na kutumia njia ambazo hazijaidhinishwa.
“Tumefanya tathmini na kuona ni busara kuanza kufunga vifaa kwenye magari ya mijini yenye changamoto hizo, hasa Dar es Salaam, kwa sababu kuna daladala nyingi na changamoto hii ni kubwa zaidi,” amesema Pazzy.
Kwa mujibu wa Latra, VTS haitumiki kudhibiti mwendo wa magari pekee, bali pia kufuatilia utekelezaji wa masharti ya leseni na kusaidia kubaini ukiukwaji unaojitokeza mara kwa mara.
Pazzy amesema matumizi ya teknolojia yameanza kuleta matokeo, kwa kuwa madereva na wamiliki wanapotambua mwenendo wa gari unaweza kufuatiliwa, huongeza utii wa sheria na kuboresha huduma kwa abiria.
Amesema masharti ya leseni yanataka watoa huduma kuzingatia nauli zilizowekwa, njia zilizoidhinishwa, usafi wa magari, matumizi ya sare na kuwafikisha abiria katika maeneo yaliyokusudiwa.
Pia, daladala zinatakiwa kuonesha wazi viwango vya nauli na njia zinazotumika ili abiria ajue kiasi anachopaswa kulipa na aweze kudai haki yake anapotozwa zaidi.
Pazzy amewataka abiria kutoshiriki katika ukiukwaji wa nauli kwa kuacha kulipa kiasi kinachotakiwa kwa mujibu wa viwango rasmi. Pia amewataka wamiliki wa daladala kuajiri madereva na makondakta wanaotambulika na Latra ili kuongeza uwajibikaji katika huduma za usafiri wa umma.
Mkazi wa Dar es Salaam, Eliya Dachi, amesema baadhi ya daladala za Mwenge-Mbezi huongeza nauli wakati wa jioni kutoka Sh800 hadi Sh1,000.
“Wao hawajali, muda ukifika jioni nauli inabadilika. Wanataka watu walipe Sh1,000 hata kama mtu anashukia njiani,” amesema Dachi.
Matilda Joseph, mkazi wa Kivule, amesema wakazi wa maeneo hayo wanapata changamoto ya usafiri kutokana na daladala nyingi zenye ruti ya Fremu 10 huishia Kivule Sokoni.
Kwa upande wake, dereva wa daladala za Gongo la Mboto, Colnell Mushi, amesema mfumo huo unaweza kusaidia, lakini Latra inapaswa kuhakikisha hatua zinazochukuliwa zinategemea ushahidi wa kutosha.
“Isije kuwa ni uonevu kwa madereva na makondakta. Tunataka ushahidi wa kutosha ili mtu asiadhibiwe kwa sababu ya malalamiko binafsi,” amesema.

