MCHUNGAJI JONAM MSANGAWALE AWATAKA WANANDOA KUTHIBITISHA UPENDO KWA VITENDO

 

Furaha na shangwe zimetawala jijini Mbeya wakati Mzee Mwangosi na Christina wakifunga ndoa na kuanza rasmi safari mpya ya maisha, katika hafla iliyohudhuriwa na ndugu, jamaa, marafiki pamoja na waumini waliokwenda kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Katika ibada hiyo ya ndoa, Mchungaji Jonam Msangawale wa Kanisa la Moravian, aliyewafungisha wanandoa hao, alitumia nafasi hiyo kutoa nasaha mbalimbali kuhusu maisha ya ndoa, akisisitiza kuwa upendo wa kweli hauishii kwenye kutamka maneno ya “nakupenda”, bali unatakiwa kuonekana kupitia matendo ya kila siku.

Msangawale alisema wanandoa wanapaswa kujifunza kuelewana na kuthibitishiana upendo kwa vitendo, ikiwemo kuhakikisha usalama, furaha na ustawi wa mwenza wao. Alisema mtu anayempenda mwenza wake anapaswa kumfikiria na kujali mahitaji yake kabla ya kuangalia mambo mengine.

“Ikiwa unajua namna gani unavyompenda mwenzako utaudhihirisha kwa matendo huo Upendo pia utahakikisha usalama wake,utahakikisha furaha yake,utahakikisha kila wakati unamfikiria yeye kabla ya kufikiria mambo mengine”

Aidha, aliwataka wanandoa kuwa na utamaduni wa kuwasiliana katika mambo madogo ya kila siku, akitoa mfano wa mmoja wao anapotoka nyumbani kwenda sokoni au sehemu nyingine Alisema ni muhimu kumjulisha mwenza wake ili kujenga heshima, uaminifu na ushirikiano ndani ya familia.

“Kwa wanandoa wote mliopo mama au baba,Mwanamke unapoondoka kwenda sokoni na mume wako yupo hapo nyumbani usiondoke tu bila kumjulisha maana anaweza kuanza kutafuta mama Fulani ameenda wapi hiyo inakuwa sio vizuri ni vizuri kutoa taarifa kwa kufahamishana kwamba kuna mahali unaenda ila hata ikitokea changamoto iwe rahisi kuweza kusaidia.”

Pia Msangawale alisisitiza umuhimu wa wanandoa kuulizana mahitaji yao badala ya kufanya maamuzi kila mmoja peke yake Alisema kuuliza mwenza anataka kula nini ni sehemu ya kuonyesha upendo na kumfanya ajisikie anathaminiwa ndani ya ndoa.

Aidha alizungumzia suala la zawadi na mavazi, akiwataka wanandoa kuelewa mahitaji na mapendeleo ya wenzao kabla ya kununua vitu kwa ajili yao Alisema zawadi inaweza kuwa ishara nzuri ya upendo, lakini ni muhimu pia kuzingatia kile ambacho mwenza anakihitaji na kukipenda.

Pia alisisitiza kuwa somo la ndoa si kwa wale wanaofunga ndoa pekee, bali ni kwa kila mmoja katika jamii, wakiwemo vijana, wazee, wajane na wale ambao bado hawajaoa au kuolewa. Alisema kila mmoja anaweza kujifunza namna ya kujenga mahusiano yenye upendo, heshima, mawasiliano na kusaidiana.

“Kila mtu ni mwanandoa mtarajiwa kwahiyo hata nyinyi mliopo hapa haya mafundisho yanawahusu usiseme kwamba mimi sipo kwenye ndoa kwahiyo haya hayanihusu hivyo kila mmoja anatakiwa ajifunze ndoa sawa na mwingine”

Hatahivyo mara baada ya ibada hiyo Msangawale aliwatakia Baraka Mzee Mwangosi na Christina kuanza maisha yao ya ndoa wakiwa na msingi wa upendo unaoonekana kwa vitendo, kuheshimiana na kusikilizana. Akisisitiza kuwa ndoa yenye furaha hujengwa na mambo madogo yanayofanywa kwa nia njema kila siku.

Karoline Leavitt Afichua Kazi Yake Mpya Baada ya Kujiuzulu White House

Global Publishers
August 22, 2026
48 views
0 Comments

Karoline Leavitt, ambaye anatarajiwa kuondoka katika nafasi yake ya Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House Press Secretary.

WASHINGTON: Karoline Leavitt, ambaye anatarajiwa kuondoka katika nafasi yake ya Msemaji wa Ikulu ya Marekani, White House Press Secretary, amefichua kuwa ataendelea kufanya kazi kwa karibu na Rais Donald Trump baada ya kuondoka serikalini.

Leavitt amesema atarejea katika MAGA Inc. mwezi Septemba, ambako awali aliwahi kufanya kazi kabla ya kuwa msemaji wa kampeni ya Trump na baadaye kuteuliwa kuwa msemaji wa Ikulu.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika safari yake ya mwisho ndani ya ndege ya Rais Air Force One kuelekea kwenye mkutano wa Trump huko South Carolina Ijumaa, Agosti 21, Leavitt alisema atatumia muda kabla ya kurejea MAGA Inc. kuwa pamoja na familia yake.

Taarifa hiyo imekuja zaidi ya wiki moja baada ya Trump kutangaza kupitia mtandao wake wa Truth Social kuwa Leavitt ataondoka katika nafasi hiyo mwishoni mwa Agosti ili kutumia muda zaidi na watoto wake wadogo na familia.

Trump alisema Leavitt ataendelea kuwa mmoja wa washauri wake wakuu akiwa nje ya Ikulu na atakuwa na ushawishi ndani ya Chama cha Republican, hasa katika kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula.

Leavitt aliwahi kufanya kazi katika MAGA Inc. kabla ya kuwa msemaji wa kitaifa wa Trump na baadaye kushika nafasi ya White House Press Secretary.

Pia amerejea kazini hivi karibuni baada ya likizo ya uzazi. Yeye na mume wake, Nicholas Riccio, walipata mtoto wao wa pili mwezi Mei.

Kwa kurejea kwake MAGA Inc., Leavitt anatarajiwa kuendelea kuwa sehemu muhimu ya timu inayomsaidia Trump kisiasa, hususan katika maandalizi ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani.

TAKUKURU Arusha yamnasa raia wa Romania kwa wizi wa fedha – HabariLeo

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imemkamata na kumweka rumande raia wa Romania, Constantin Podoleanu (39), kwa tuhuma za wizi wa mamilioni ya fedha kupitia taarifa za kadi za benki na kujipatia fedha kwa njia haramu.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 20 mwaka huu majira ya saa 4 usiku katika nyumba yake iliyopo Njiro Block D, Kata ya Engutoto, Halmashauri ya Jiji la Arusha, ambapo maafisa wa TAKUKURU walifanya upekuzi na kubaini vifaa mbalimbali vinavyodaiwa kutumika katika uhalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amesema katika upekuzi huo mtuhumiwa alikutwa na mashine sita za POS, kadi mbalimbali za benki, vifaa na kemikali zinazodaiwa kutumika kutengeneza kadi bandia, pamoja na kompyuta mpakato mbili.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa raia huyo wa Romania alikuwa amefungua karakana ya kufanyia shughuli za uhalifu nyumbani kwake.

Ngailo amesema pia katika upekuzi huo zilikutwa stakabadhi mbalimbali za malipo, zikiwemo zenye thamani ya takribani Sh milioni 171.7 na nyingine za malipo ya dola za Marekani 55,987.20.

Aidha, amesema TAKUKURU ilikuta fedha taslimu za Tanzania kiasi cha Sh milioni mbili, noti za Euro 20 pamoja na fedha za Saudi Arabia kiasi cha Riyal 15.

Kwa mujibu wa Kamanda Ngailo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa taarifa za kadi hizo za benki zilizoibwa zilihusisha raia wa mataifa mbalimbali nje ya Tanzania, ambao fedha zao zilikuwa zikitolewa kwenye akaunti zao na baadaye kuonekana zimetumika kulipia huduma mbalimbali nchini Tanzania, licha ya wahusika kutowahi kupata huduma hizo katika kipindi husika.

Amesema TAKUKURU Mkoa wa Arusha inaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli na mazingira yote ya tukio hilo, na kwamba hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Aidha, TAKUKURU imewataka wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kufichua vitendo vya uhalifu, ikisisitiza kuwa hakuna mhalifu atakayekuwa salama popote atakapojificha, ndani au nje ya nchi.

TAKUKURU imesema itaendelea kuwafuatilia wahalifu na kuhakikisha wanakamatwa ili wakabiliwe na mkono wa sheria.

Messi Afikisha Mabao 922, Historia Yazidi Kuandikwa Marekani

Global Publishers
August 22, 2026
402 views
0 Comments

MIAMI, Marekani — Nyota wa Argentina, Lionel Messi, ameendelea kuweka historia katika soka baada ya kufikisha jumla ya mabao 922 katika maisha yake ya soka.

Messi alifikia idadi hiyo baada ya kufunga bao lake la 70 katika Ligi Kuu ya Marekani (MLS) akiwa na Inter Miami, katika mchezo uliomalizika kwa sare ya 2-2 dhidi ya Philadelphia Union.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 39 alifunga bao hilo dakika ya 60, likiwa moja ya mabao yaliyomsaidia kuendelea kuongeza rekodi zake katika soka la Marekani.

Bao hilo limeongeza rekodi ya Messi tangu alipohamia Inter Miami, ambapo ameendelea kuonyesha kiwango cha juu licha ya kuwa katika hatua ya mwisho ya safari yake ya soka.

Kwa kufikisha mabao 70 katika MLS, Messi anaendelea kuweka alama katika ligi hiyo na kuongeza idadi ya rekodi binafsi ambazo ameweka tangu kuanza kucheza soka la kulipwa.

Hata hivyo, bao hilo limekuja baada ya kipindi ambacho Messi amekuwa akikabiliwa na changamoto katika kiwango chake binafsi, lakini bado ameendelea kuwa miongoni mwa wachezaji wenye ushawishi mkubwa katika timu yake.

Messi ameendelea kuongeza idadi ya mabao katika kila hatua ya safari yake ya soka, akitengeneza rekodi ambazo zimekuwa sehemu ya mjadala mkubwa kuhusu nafasi yake miongoni mwa wachezaji bora zaidi kuwahi kucheza mchezo huo.

Kwa kufikisha mabao 922, macho ya mashabiki sasa yataendelea kuwa kwake kuona kama ataweza kuvuka hatua nyingine kubwa katika mbio zake za kuongeza idadi ya mabao kabla ya kutundika daruga.

Na Mputa Ngaga, GPL- TUDACO

Ratiba ya Mzunguko wa Tatu NBC Premier League 2026/27

Global Publishers
August 22, 2026
54 views
0 Comments

Ligi Kuu ya NBC Premier League msimu wa 2026/27 inaendelea, huku timu zikijiandaa kushuka dimbani katika mzunguko wa tatu kwa ajili ya kusaka pointi muhimu.

Baada ya michezo miwili, Yanga SC wanaongoza msimamo wakiwa na pointi sita, huku safu yao ya ushambuliaji ikiwa imefunga jumla ya mabao saba.

Kwa upande mwingine, Coastal Union ya Tanga ndiyo inayoshika mkia baada ya kupoteza michezo yake miwili ya mwanzo. Timu hiyo ilianza kwa kupoteza nyumbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani dhidi ya Mashujaa, kabla ya kufungwa tena ugenini na Yanga SC kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Hii ndiyo ratiba ya michezo ya mzunguko wa tatu:

  • Singida Black Stars vs Simba SC — Agosti 22, 2026, Uwanja wa Airtel, saa 12:00 jioni.
  • Geita Gold vs Kagera Sugar — Agosti 22, 2026, Uwanja wa Bukombe, saa 2:30 usiku.
  • Mbeya City vs Mashujaa FC — Agosti 23, 2026, Uwanja wa Sokoine, saa 10:00 jioni.
  • Azam FC vs Pamba Jiji FC — Agosti 23, 2026, Uwanja wa Azam Complex, saa 1:00 usiku.
  • Yanga SC vs JKT Tanzania — Agosti 24, 2026, Uwanja wa KMC Complex, saa 12:00 usiku.
  • Coastal Union vs TRA United — Agosti 24, 2026, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, saa 2:00 usiku.
  • Namungo FC vs Fountain Gate — Agosti 25, 2026, Uwanja wa Majaliwa, saa 12:00 jioni.
  • Dodoma Jiji FC vs Polisi Tanzania — Agosti 25, 2026, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, saa 2:30 usiku.

Mzunguko huo unatarajiwa kutoa ushindani mkubwa, hasa kwa timu zinazolenga kuendelea kujiimarisha katika nafasi za juu na zile zinazotafuta pointi za kwanza za msimu.

JNHPP kuipa Tanzania nafasi mpya biashara za kikanda – HabariLeo

PWANI: Serikali inalenga kutumia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ( JNHPP) kuongeza uzalishaji wa umeme na kuiweka Tanzania katika nafasi muhimu ya kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Mkurugenzi wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema mradi huo umejengwa katika eneo la Mto Rufiji na umebuniwa kuwa na mitambo tisa ya kuzalisha umeme.

Twange amesema jumla ya mitambo hiyo tisa imebuniwa kuzalisha megawati 2,115, hatua ambayo itaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa Tanzania katika uzalishaji wa umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi na biashara.

Amesema Serikali kupitia TANESCO ilisaini mkataba wa ujenzi wa mradi huo tarehe 12 Desemba 2018 na kampuni za Arab Contractors na Elsewedy Electric, zote kutoka Misri, huku siku moja kabla, tarehe 11 Desemba 2018, Serikali ikimkabidhi TANESCO jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, amesema tarehe 17 Aprili 2019 TANESCO ilisaini mkataba na TANROADS kwa ajili ya masuala ya ushauri na usimamizi wa baadhi ya shughuli za mradi.

Kwa mujibu wa Twange, Bwawa la Mwalimu Nyerere ni mradi mkubwa wa kihandisi wenye miundombinu ya kisasa na ya kimkakati, ukiwa na vipengele sita muhimu vinavyounda kituo hicho cha kuzalisha umeme.

Ameeleza kuwa bwawa hilo lina uwezo wa kuhifadhi maji takribani mita za ujazo bilioni 32.784, huku maji yanayoingia kwenye bwawa yakitokana na vyanzo vikuu vitatu ambavyo ni Mto Kilombero unaochangia asilimia 65, Mto Luwegu asilimia 19 na Mto Ruaha asilimia 15.

TAG NA EAGT ZAFUNGUA UKURASA MPYA BAADA YA MGOGORO WA MIAKA 40

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Dodoma

BAADA ya zaidi ya miongo minne ya kutokubaliana, Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) na Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) zimefikia makubaliano ya kuhitimisha tofauti zao, hatua iliyofikiwa kupitia kusainiwa kwa hati rasmi ya makubaliano jijini Dodoma.

Mzozo huo ulijitokeza kufuatia mgawanyiko wa mwaka 1980, na kwa miaka iliyofuata ukahusisha masuala mbalimbali yaliyohitaji suluhu, ikiwemo namna ya kushughulikia mali zilizokuwa chini ya taasisi hizo.

Hatua ya sasa imekuja baada ya viongozi wa makanisa hayo kukaa pamoja na kufikia muafaka unaolenga kuweka kikomo cha tofauti hizo na kuruhusu kila upande kuendelea na shughuli zake bila mvutano wa muda mrefu.

Miongoni mwa mambo yaliyoainishwa katika makubaliano hayo ni utaratibu wa kushughulikia na kugawana mali zilizohusishwa na mgogoro huo, jambo ambalo limekuwa sehemu ya mjadala kati ya pande hizo kwa muda mrefu.

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Askofu Mkuu wa TAG, Askofu Dkt. Barnabas Mtokambali, amesema kufikiwa kwa makubaliano hayo ni hatua yenye umuhimu mkubwa kwa taasisi hizo na waumini wake, baada ya kipindi kirefu cha kutafuta suluhu.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa EAGT, Askofu Prof. Brown Mwakipesile, amesema makubaliano hayo yanaashiria mwanzo wa mahusiano mapya kati ya makanisa hayo, huku akieleza umuhimu wa pande zote kuheshimu na kutekeleza yaliyokubaliwa.

Baadhi ya viongozi na waumini wa makanisa hayo, akiwemo Mchungaji Isaya Ikili na Mchungaji Ayubu Mtula, wamepokea hatua hiyo kwa furaha, wakisema inatoa fursa ya kuimarisha umoja na kuondoa tofauti zilizodumu kwa muda mrefu.

Wamesema suluhu hiyo inapaswa kuwa msingi wa kujenga mahusiano mazuri zaidi na kuendeleza huduma za makanisa hayo kwa waumini na jamii kwa ujumla, badala ya kuendelea kutumia nguvu na muda katika tofauti za zamani.

Kwa kusainiwa kwa hati hiyo jijini Dodoma, TAG na EAGT sasa zimeweka rasmi msingi wa kuhitimisha mgogoro huo wa muda mrefu, huku utekelezaji wa makubaliano kuhusu mali na masuala mengine yaliyokubaliwa ukitarajiwa kufungua ukurasa mpya katika historia ya makanisa hayo.

Rais Samia Akutana na Msanii Mkongwe Yvonne Chaka Chaka

Global Publishers
August 22, 2026
60 views
0 Comments

DAR ES SALAAM: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na msanii mkongwe kutoka Afrika Kusini, Yvonne Chaka Chaka, katika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Samia alizungumza na msanii huyo tarehe 20 Agosti 2026, katika mazungumzo yaliyofanyika wakati Chaka Chaka akiwa nchini Tanzania kwa ajili ya kushiriki katika Jukwaa la Mashariki Creative Expo 2026.

Jukwaa hilo linalenga kutoa elimu pamoja na kuhamasisha ulinzi wa kazi za ubunifu, likijumuisha maeneo mbalimbali kama filamu, sanaa za ufundi na muziki.

Ushiriki wa msanii huyo mkongwe katika jukwaa hilo unaongeza fursa ya kubadilishana uzoefu na maarifa katika sekta ya ubunifu, huku wadau wakijadili namna ya kulinda na kuendeleza kazi za wasanii.

Chaka Chaka ni miongoni mwa wasanii wakubwa wa Afrika Kusini waliojenga jina kwa muda mrefu katika muziki wa bara hilo na amekuwa akihusishwa pia na shughuli mbalimbali za kijamii na kibinadamu.

Kukutana kwake na Rais Samia kunakuja wakati Tanzania ikiendelea kuimarisha nafasi ya sekta ya ubunifu katika kukuza vipaji, ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana na wasanii.

Freeman Mbowe Aonekana Kwenye Uzinduzi wa Kituo cha Julius Nyerere

Global Publishers
August 22, 2026
78 views
0 Comments

RUFIJI, PWANI: Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe, amewasili katika hafla ya uzinduzi rasmi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP).

Kituo hicho, kinachopatikana katika eneo la mradi wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani, kina uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati 2,115 za umeme.

Uzinduzi huo ni sehemu ya hatua muhimu katika sekta ya nishati nchini Tanzania, huku mradi wa JNHPP ukilenga kuongeza uzalishaji wa umeme na kusaidia kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati nchini.

Mbowe ni miongoni mwa viongozi na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo, ambayo imewakutanisha wadau na viongozi katika eneo la mradi wa Julius Nyerere.

Kituo hicho kinatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza upatikanaji wa umeme na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.

TTCL YALENGA KAYA ZAIDI 400,000 KATIKA AWAMU MPYA YA FAIBA MLANGONI KWAKO

 

Na Matukio DaimaMedia 

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeanza utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako (Fiber to the Home–FTTH), likilenga kuongeza zaidi ya Home Pass 400,000 ili kupanua upatikanaji wa intaneti yenye kasi kwa wananchi, taasisi na wafanyabiashara nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa awamu hiyo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema Serikali inataka huduma hiyo ifike katika maeneo yenye makazi yanayokua, masoko, maeneo ya biashara, viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema mafanikio ya mradi huo hayataangaliwa kwa idadi ya miundombinu itakayojengwa pekee, bali pia kwa wananchi watakaounganishwa, ubora na kasi ya intaneti pamoja na kiwango cha kuridhika kwa wateja.

“Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako si ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano pekee, bali ni hatua ya kimkakati ya kufungua fursa za elimu, biashara, ajira na ubunifu, na kuchochea ujenzi wa uchumi wa kidijitali nchini,” amesema.

Waziri Kairuki ameitaka TTCL kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa ubora, uhakika na gharama zinazomudu wananchi, huku ikiboresha mifumo ya huduma kwa wateja, hasa katika kushughulikia malalamiko kwa wakati na kwa ufanisi.

Aidha, ameagiza shirika hilo kuandaa vifurushi vinavyokidhi mahitaji na uwezo wa makundi mbalimbali, yakiwemo familia, wanafunzi, vijana na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, utekelezaji wa mradi huo pia unatakiwa kusimamiwa kwa kuzingatia uwajibikaji na nidhamu ya kibiashara, huku wazabuni na wakandarasi wakihakikisha kazi zinakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha inayowekezwa.

Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali wa mwaka 2024–2034, unaolenga kuongeza matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa huduma za Serikali kwa njia za kidijitali.

Ameeleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka huo angalau asilimia 70 ya wananchi wanatumia TEHAMA, huku zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali zikitolewa kwa njia ya kidijitali iliyo salama na jumuishi.

Akizungumzia hali ya matumizi ya intaneti nchini, Waziri Kairuki ametumia takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa robo mwaka iliyoishia Juni 2026, akisema usajili wa intaneti ulifikia 62,793,986, wakati matumizi ya data yalifikia Petabaiti 1,041.

Hata hivyo, amesema idadi ya usajili wa huduma ya Faiba Nyumbani ilikuwa 178,904, jambo linaloonyesha kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuongeza matumizi ya intaneti ya kasi kupitia teknolojia ya nyuzi za macho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema kuanza kwa Awamu ya Pili ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Biashara wa Miaka 10 wa shirika hilo kwa kipindi cha 2025/26 hadi 2034/35.

Marwa amesema TTCL imefikia hatua hiyo ikiwa tayari imejenga msingi kupitia Awamu ya Kwanza ya mradi huo, ambapo shirika limefanikiwa kujenga zaidi ya Home Pass 280,000 na kufikisha jumla ya maungio ya huduma ya nyuzi za macho karibu 300,000 nchini.