mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) Keneth Simbaya (wa tatu kushoto ) akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Kilolo Fredy Mwakibete aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Iringa katika mkutano wa baraza la Habari Tanzania (MCT) jana wakati wa mkutano mkuu wa 28 wa taasisi hiyo huku UTPC ikipongezwa kwa kulipa ada kwa wakati (Picha na Matukio Daima Media
NA MATUKIO DAIMA MEDIA
IRINGA.
Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeeleza mikakati ya kuimarisha uhai wa wanachama wake kwa kuboresha mfumo wa ada na kuanzisha vifurushi vya huduma vitakavyowawezesha wanachama kunufaika na mafunzo, msaada wa kisheria, usalama wa kimwili na kidijitali pamoja na fursa mbalimbali za kitaaluma.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 28 wa MCT uliofanyika mkoani Iringa, Katibu Mtendaji wa baraza hilo Ernest Sungura amesema changamoto zilizokuwepo kwa muda mrefu ni pamoja na mfumo wa ada ambao haukuwa ukitoa thamani ya moja kwa moja kwa wanachama pamoja na madeni yasiyo na tija, hali iliyosababisha taasisi hiyo kuweka mikakati mipya ya kuimarisha uendeshaji wake.
“Uimara wa MCT haupimwi kwa idadi ya wanachama pekee, bali ushiriki wao katika shughuli za baraza, uwajibikaji na manufaa wanayopata kupitia uanachama, akisisitiza kuwa wanachama wanapaswa kuona thamani ya huduma wanazopata ili waweze kuchangia ada kwa wakati na kwa hiari”alisema
Katika hatua nyingine, MCT imezindua kampuni tanzu ya Media Integrity Consulting Services, itakayokuwa mkono wa kibiashara wa baraza hilo kwa kujihusisha na tafiti za vyombo vya habari, ushauri wa mawasiliano, mafunzo ya kulipia, usimamizi wa matukio na huduma za ushauri, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa ada na misaada ya wahisani.Ameeleza kuwa kampuni hiyo itatumia eneo la ardhi lenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 65,000 lililopo Bagamoyo kwa shughuli za uwekezaji na uzalishaji, huku akiwahimiza wanachama na wawekezaji wengine kushiriki katika fursa zitakazotokana na eneo hilo kupitia ubia na uwekezaji wa pamoja.
Aidha, amesema MCT imeendelea na mazungumzo na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ili kupata uelewa wa fursa za uwekezaji zinazoweza kutekelezwa katika eneo hilo, huku wawakilishi wa mamlaka hiyo wakitarajiwa kutoa maelezo kuhusu fursa zilizopo kwa wanachama.
Akizungumzia mustakabali wa taasisi hiyo, Sungura amewataka wanachama kutambua kuwa viongozi na bodi zinazochaguliwa huwa na muda maalumu wa uongozi, lakini wanachama ndio msingi wa kudumu wa taasisi hiyo. Amewataka kutumia umoja wao kushiriki katika uwekezaji na kufanya maamuzi yatakayolinda maslahi ya MCT kwa muda mrefu.
“Nawahimiza wanahabari kuendelea kuzingatia maadili, kuwajibika katika ukusanyaji na utoaji wa taarifa pamoja na kulinda heshima ya taaluma, uhuru wa habari hauwezi kudumu bila uwajibikaji na mifumo imara ya kujisimamia, Aidha, natoa wito kwa wajumbe wa mkutano huu kujadili kwa uwazi na kuweka maazimio yatakayotekelezeka kwa maslahi ya taasisi na tasnia ya habari kwa ujumla”alisema
Awali akifungua Mkutano huo Mkuu wa 28 wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) uliofanyika mkoani Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Fredy Atupele Mwakibete kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James amewaasa wanahabari kuzingatia maadili na weledi wa taaluma ya habari kwa kutoa taarifa sahihi, za ukweli na kuepuka kusambaza habari za uongo na upotoshaji, huku akisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mazingira salama yatakayowawezesha waandishi kutekeleza majukumu yao bila hofu.
“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuunganisha serikali na wananchi kwa kutoa elimu, kuhamasisha maendeleo na kusimamia uwajibikaji, hivyo amewataka wanahabari kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya taaluma”alisema
Aidha, ameipongeza MCT kwa kuanzisha kampuni tanzu ya Media Intelligence Consulting Services, akieleza kuwa serikali ipo tayari kushirikiana nayo kwa kutumia huduma za utafiti na ushauri. Pia ameitaka taasisi hiyo kutumia eneo lake lenye ukubwa wa zaidi ya mita za mraba 65,000 lililopo Bagamoyo kwa uwekezaji na shughuli za uzalishaji zitakazoongeza mapato ya taasisi.
Akizungumzia fursa za Mkoa wa Iringa, amewahimiza wanahabari kutumia kalamu na taaluma zao kutangaza vivutio vya utalii na miradi ya maendeleo, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Makumbusho ya Mkwawa, miradi ya umwagiliaji ya Isakalilo, ujenzi wa barabara ya mchepuo wa Igumbilo–Ihemi pamoja na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Iringa.
Kwa upande wake Mratibu wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani Deusdedit Hokororo –TISEZA amesema wametambua mchango wa vyombo vya habari katika kuhamasisha uwekezaji nchini, ikieleza kuwa waandishi wa habari wamekuwa wadau muhimu katika kufikisha taarifa za fursa za uwekezaji kwa wananchi na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Hokororo amesema mafanikio yaliyopatikana katika kusajili zaidi ya miradi 3,500 ya uwekezaji yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali, wakiwemo wanahabari ambao wamekuwa wakitangaza fursa na kuelimisha jamii kuhusu masuala ya uwekezaji.
“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuhamasisha uwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwemo viwanda na usindikaji wa madini, hivyo kuwataka waandishi kuendelea kutumia maarifa na uzoefu wao kutangaza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji”alisema
Aidha, ameeleza kufurahishwa na taarifa za MCT kumiliki eneo kubwa la ardhi Bagamoyo, lililopo karibu na eneo la uwekezaji la Bagamoyo, akiwahimiza viongozi na wanachama wa baraza hilo kulitumia eneo hilo kama fursa ya kujenga miradi itakayowaongezea kipato na kuimarisha taasisi yao.
Amesema TISEZA ipo tayari kushirikiana na MCT katika kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuunganisha taasisi hiyo na wawekezaji pamoja na kusaidia kuweka mazingira yatakayowezesha eneo hilo kutumika kwa shughuli za kiuchumi kupitia uwekezaji wa moja kwa moja au ubia.







































