NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Jenerali Salim Saleh amesema ameanza kushughulikia suala linalomhusu mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Dkt. Kizza Besigye, baada ya ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini humo, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Akizungumza Oktoba 30, 2026, na viongozi wa Bunge pamoja na wabunge katika eneo la Kapeeka, Wilaya ya Nakaseke, Saleh amesema hatua hiyo imewezesha kurejesha mawasiliano kati yake na Besigye baada ya kutengana kwa muda kutokana na tofauti za kisiasa.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor, Saleh amesema alimtembelea Besigye na kukuta hali yake ya afya ikiwa mbaya, kabla ya kusaidia kuratibu uhamisho wake kwenda katika kituo cha matibabu cha Joint Clinical Research Centre kilichopo Lubowa.
Saleh ameeleza kuwa mawasiliano yao yanaweza kufungua njia ya mazungumzo ya pamoja kuhusu mustakabali wa Uganda ndani ya miezi mitatu hadi sita ijayo. Hata hivyo, hakufafanua kama mazungumzo hayo ni sehemu ya mpango rasmi wa amani au hatua za kuanzisha makubaliano ya kisiasa kuhusu kuachiwa kwa Besigye.
Kwa upande wake, mke wa Besigye, Winnie Byanyima, amesisitiza kuwa afya na haki za mumewe hazipaswi kuwa sehemu ya majadiliano ya kisiasa, akitaka apewe dhamana pamoja na huduma bora za matibabu.

