KILIMO CHACHOCHEA AJIRA, MAPATO YA SERIKALI KIGOMA

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

MPANGO wa serikali  mkoani Kigoma kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kubadili shughuli za kilimo kuwa biashara kimeifanya sekta hiyo kuchangia kuongeza mapato ya serikali sambamba na kuvutia watu wengi kujiingiza kwenye shughuli za kilimo kama ajira rasmi.

Katibu Tawala Msaidizi huduma za uchumi na uzalishaji katika sekretariet ya mkoa kigoma, James Pater alisema hayo wakati Mkurugenzi  Mkazi wa Shirika la maendeleo la serikali ya Korea (KOICA), Kim Sik Hyun alipofanya ziara na kutembelea mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KITIKI) ambao unafadhiliwa na Shirika hilo kwa ushirikiano na Shirika la Chakula la Umoja lwa Mataifa (WFP).

 

Peter alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu kilimo kimeongeza mapato ya serikali kwa asilimia 44 huku sekta hiyo ikikua kwa  asilimia 17 na kusababisha kuongezeka kwa uzalishaji na matumizi ya pembejeo ikiwemo mbolea na mbegu bora kwa wakulima kwa  asilimia 11.3 hivyo kukifanya kilimo kuwa moja ya sekta za kimkakati katika masuala ya uchumi na biashara mkoani Kigoma kutoka kwenye kilimo cha kujikumu na kuwa biashara.

 

Mtaalam huyo wa kilimo alisema kuwa baada ya kuongezeka kwa uzalishaji kuliibuka chngamoto ya soko na ndipo mradi wa Kilimo Tija Kigoma (KITIKI) ukaanza kutekelezwa na kusaidia kukabili changamoto ya soko na hivyo kukifanya kilimo ambacho ndiyo shughuli kubwa ya kiuchumi ya wananchi wa  mkoa Kigoma kuwa tegemeo kubwa kama  ajira yao rasmi.

 

Akizungumzia kufanyika kwa mradi huo Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini, Kim Sik Hyum alisema kuwa mradi huo umekuwa kichocheo kikubwa katika kuboresha kilimo mkoani Kigoma na kuimarisha uchumi wa wakulima wa dogo ili kukua na kukifanya kilimo kuwa shughuli kuu ya kiuchumi mkoani humo.

Kwa upande wake Mkurugenzi  Mkazi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, Ronald Tran Ba Huy alisema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa Mradi wa KITIKI Shirika hilo lilikuwa likiagiza chakula mikoa mbalimbali kwa ajili ya wakimbizi mkoani Kigoma lakini kwa sasa baada ya kuanza mradi huo na wakulima kujengewa uwezo Shirika hilo linanunua sehemu kubwa ya mahindi na maharage kwa wakulima wa mkoa Kigoma. 

Mwisho.